• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 AM
Allegri au Xavi kutua Barca endapo kocha Ernesto atatimuliwa

Allegri au Xavi kutua Barca endapo kocha Ernesto atatimuliwa

Na MASHIRIKA

BARCELONA, Uhispania

MSURURU wa matokeo duni ya Barcelona katika mechi za ugenini katika kipute cha Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) huenda ukamshuhudia kocha Ernesto Valverde akitemwa na waajiri wake.

Baada ya kulimwa 2-0 na limbukeni Granada mwishoni mwa wiki jana, Valverde alikiri kwamba hatima yake ugani Camp Nou imesalia kuning’inia padogo na huenda presha ya kujinyanyua kwa Barcelona ikawazamisha hata zaidi katika mechi zijazo.

Hata hivyo, mkufunzi huyo mzawa wa Uhispania alikariri kwamba ndiye anayestahili kulaumiwa kwa matokeo mabaya ya kikosi chake.

Kulingana na gazeti la ‘Mundo Deportivo’ nchini Uhispania, kikubwa zaidi ambacho bado kinamweka Valverde kambini mwa Barcelona ni uungwaji mkono anaojivunia kutoka kwa nahodha Lionel Messi.

Mwishoni mwa mechi dhidi ya Granada, Valverde alishambuliwa pakubwa na mashabiki wa Barcelona mitandaoni huku sehemu kubwa ikitaka atimuliwe kwa kushindwa kuimarisha safu ya ulinzi ya kikosi hicho.

Kwa mujibu wa Mundo, huenda mchuano wa leo wa La Liga ukawa wa mwisho kwa Valverde kusimamia kambini mwa Barcelona watakaowaalika Villarreal ambao watashuka dimbani wakijivunia hamasa ya kuwapepeta Real Madrid msimu huu.

Iwapo Valverde atapigwa kalamu, magazeti mengi nchini Uhispania yanabashiri kwamba nafasi yake huenda ikatwaliwa ama na Pablo Machin, Quiqe Setien, Abelardo, Massimiliano Allegri, Laurent Blanc au hata Jose Mourinho japo kocha huyu wa zamani wa Chelsea na Manchester United anahusishwa na uwezekano mkubwa wa kurejea kambini mwa Real Madrid iwapo miamba hao wa Uhispania wataagana na Zinedine Zidane.

Marcelino ambaye alitimuliwa majuzi na Valencia angalikuwa pazuri zaidi kumrithi Valverde kambini mwa Barcelona ila kanuni za soka ya Uhispania hazimruhusu.

Kwa mujibu wa sheria za ligi hiyo, kocha mmoja hawezi akadhibiti mikoba ya vikosi viwili tofauti vya La Liga katika kipindi cha msimu mmoja.

Kati ya wakufunzi ambao tayari wana kazi, Ronald Koeman ambaye anawanoa vijana wa timu ya taifa ya Uholanzi ndiye anayepigiwa upatu wa kutua Barcelona kwa urahisi kwa kuwa ni mchezaji wa zamani wa kikosi hicho.

Mwingine ni nyota wa zamani wa klabu hiyo, Xavi Hernandez ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya kikosi cha Al Sadd nchini Qatar.

Xavi tayari amedokeza ukubwa wa kiu yake ya kuwanoa nyota Lionel Messi, Luis Suarez, Sergio Busquets na Antoine Griezmann uwanjani Camp Nou.

Historia mbovu

Ushindi wa Granada uliwafanya Barcelona kuwa na historia mbovu zaidi kwenye La Liga katika kipindi cha miaka 25 iliyopita.

Kwa sasa wanajivunia alama saba pekee sawa na Levante na Osasuna ambao pia waliambulia sare tasa dhidi ya Eibar na Real Betis mtawalia.

Rekodi ya Barcelona katika kampeni za La Liga kwa sasa ndiyo mbovu zaidi kuwahi kushuhudiwa na kikosi hicho tangu 1994-95 chini ya aliyekuwa mkufunzi wao, Johan Cruyff.

Barcelona wamejivunia ufanisi wa kunyanyua mataji manne ya La Liga katika kipindi cha misimu mitano iliyopita.

Hata hivyo, wamepoteza mechi mbili za ufunguzi kati ya tano zilizopita.

Msimu jana, miamba hawa wa soka ya Uhispania walizidiwa maarifa katika mechi tatu pekee kati ya 38 za muhula Mzima ligini.

Ubovu wa rekodi ya Barcelona kila wanapocheza nje ya uwanja wa Camp Nou kwa sasa umewashuhudia wakishindwa kujivunia ushindi wowote ugenini tangu Aprili 2019.

You can share this post!

KIVUMBI CARABAO: Patashika Carabao Cup iking’oa nanga

Gor Mahia walilia msaada wa fedha tena

adminleo