Wanawake 60 wenye Fistula wapata matibabu ya bure Thika Level Five
Na LAWRENCE ONGARO
WANAWAKE wapatao 60 wamenufaika kwa kupewa matibabu ya bure ya urekebeshaji wa matatizo ya Fistula katika hospitali ya Thika Level Five.
Wakati wa shughuli hiyo ya Jumatatu, madaktari watatu, wauguzi 20 na wahudumu 40 wa afya ya jamii (community health workers) walishiriki huku wanawake hao wakipongeza hatua hiyo kuwa ya ukombozi kwao.
Dkt Betty Kasioka aliyekuwa kinara wa shughuli hiyo, alisema kwa muda mrefu wanawake wamekuwa katika shida kubwa zinazosababishwa na shida hiyo ya Fistula.
“Wanawake wengi wamepata shida kubwa – ya kwenda haja ndogo na hata kubwa – kwa sababu ya matatizo ya viungo vya uzazi ambavyo huwa vimetoneshwa wakati huo wa kujifungua,” alisema Dkt Kasioka.
Alisema mara nyingi wanawake wanaojifungua watoto mashinani huwa na matatizo mengi ya kujifungua na katika hali hiyo, sehemu ya kupitisha mtoto na sehemu ya kupitisha mkojo hutoneshwa. Baadaye kuacha matundu katika maeneo hayo.
Bi Nduta Nyambura ambaye ni msusi mjini Thika anasema baada ya kujifungua mtoto alipata matatizo hayo ya Fistula.
“Hata mume wangu hangeketi karibu na mimi kutokana na harufu mbaya kutoka kwa mwili wangu. Nilikuwa naenda haja bila kujizuia na hali hiyo ilinitatiza kwa muda mrefu,” alisema Bi Nyambura.
Uvundo
Alisema hata wakati fulani akiwa pahala pake pa kazi, wateja walisita kufika hapo kwa sababu hawangevumilia harufu mbaya iliyokuwa ikienea mahali hapo.
Bi Angeline Mutio wa kutoka Embu naye alisema muda wa miezi chache ambayo imepita, alipitia masaibu kwa sababu alipojifungua alipata matatizo kadha katika nyungu yake ya uterus.
“Baadaye niliwahiwa katika hospitali kuu ya Thika Level 5 ili kufanyiwa uchunguzi zaidi,” alisema Bi Mutio na kuongeza kwamba iligundulika tayari alikuwa na Fistula.
Kulingana na Dkt Jackline Njoroge ni kwamba katika nchi ya Kenya kuna upungufu wa madaktari wenye ujuzi wa upasuaji wa Fistula.
“Kwa hivyo inakuwa ni vigumu kwa wanawake walio vijijini kupata huduma ya dharura iwapo watapitia masaibu hayo. Ni vyema kuwe na hamasisho kila mara kwa wanawake hasa mashinani ili waweze kujua namna ya kufika hospitali mapema kabla ya kujifungua mtoto,” alisema Dkt Njoroge.
Alisema hali hiyo inaweza kuangamizwa iwapo wanawake watakuwa wakihudhuria hospitali kwa ushauri kila mara wanapokuwa wajawazito.
Alisema kuwa kote ulimwenguni, utafiti umebainisha kuwa zaidi ya wanawake 2 milioni hupata matatizo ya Fistula kila mwaka huku nchi ya Kenya ikirekodi idadi ya wanawake 3,000 kila mwaka.