Habari Mseto

MIMBA: 'Wasichana Wetu Wafaulu' ni mpango unaowawezesha wasichana kusalia shuleni

September 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MAGDALENE WANJA

SHIRIKA la Ustawishaji Elimu (EDT) limebuni mpango wa kuwawezesha wasichana kusalia shuleni; hasa waliopata mimba wangali wadogo kiumri.

Mpango huo unaofahamika kama ‘Wasichana Wetu Wafaulu’ tayari umeanza katika mbalimbali katika kaunti nane ambapo katika miji ya Nairobi na Mombasa, sehemu ambazo zimepewa zingatio ni mitaa duni.

Mkurugenzi wa sera na ushirikiano Dkt Sylvester Mulambe alisema kuwa, serikali ikishirikiana na shirika hilo imeanzisha mpango huo ili kuhakikisha kuwa waschana wanaso,ma kuanzia shule ya msingi hadi sekondari bila matatizo yoyote.

Dkt Mulambe alizungumza baada ya kuzuru shule ya Likoni School for the Visually Impaired Children (VIC) na ile ya upili ya St Thomas Girls wiki jana.

“Ushirikiano huu umechangia pakubwa katika ongezeko la idadi ya wasichana ambao wamerudi shuleni kuendelea na masomo hasa baada ya kupata mimba za mapema,” akasema Dkt Mulambe.

Naibu mkurugenzi wa shirika la Girls’ Education Challenge (GEC) Bi Margaret Kamau alisema kuwa mradi huo ambao umefadhiliwa na shirika la GEC unasaidia katika kuinua hali ya masomo ya wasichana katika maeneo ya Nairobi, Mombasa, Kwale, Kilifi, Tana River, Turkana, Samburu na Marsabit.

Alisema kuwa mradi huo umewasaidia wasichana waliopata mimba za mapema kifedha na kuwapa ushauri.