NDIVYO SIVYO: Tuache huu ulipyoto wa kauli kama vile ‘nimeshinda niki…’
Na ENOCK NYARIKI
WATU wanaposema “nimeshinda nikimwambia…”; “nimeshinda nikimwonya…” au “nimeshinda nikimshauri…” kauli hizo hufanikisha mawasiliano ya “barabarani” tu wala si sahihi kisarufi.
Kitenzi “shinda” hakiwezi kamwe kutumiwa kuonyesha kuwa kitendo kimekuwa kikitendeka kwa muda mrefu, kikirudiwarudiwa au kikitendeka kila baada ya muda mfupi. Aidha, kitenzi hicho hakipaswi kutumiwa katika nafasi ya kitenzi (-wa).
Tutaonyesha maneno au kauli ambazo zinapaswa kutumiwa katika mazingira hayo ila kwanza ni muhimu kuangazia maana ya “shinda”.
Neno shinda hutumiwa kama kitenzi au kivumishi. Kama kivumishi huibua dhana ya kutojaa kwa chombo. Hapa ndipo panapochimbuka msemo maarufu wa debe shinda haliachi kutika.
Katika makala yetu, tutaegemea zaidi matumizi ya neno shinda kama kitenzi. Kitenzi hicho hutumiwa kueleza kitendo cha kukaa mahali kwa siku nzima.
Mfano: Baba ameshinda shuleni kwa mwanawe leo. Kauli “shinda” yamkini ndiyo pia watu huitumia kwa maana ya ‘muda mwingi”. Kwa hivyo, wanaposema “nimeshinda nikimweleza” neno shinda, katika kauli hiyo, hudhaniwa kuwa na maana ya kutumia wakati mwingi kumweleza, kukirudiarudia kitendo chenyewe au kukitenda kila baada ya muda mfupi. Ifahamike kuwa hata pale ambapo kitenzi shinda hutumiwa katika salamu “umeshindaje?” huibua wazo la “umekuwa katika hali gani?”
Dhana ya wakati haijitokezi hapa ingawa hakika salamu za “umeshindaje” huzingatia wakati. Mathalani, mtu hawezi kuulizwa ameshindaje wakati wa asubuhi.
Kitenzi shinda pia hutumiwa kwa maana ya kufaulu katika jambo fulani kwa mfano mtihani au mchezo.
Hata hivyo, nia ya mzungumzaji iwapo ni kueleza kuwa jambo fulani limekuwa likiendelea kwa muda mrefu, matumizi ya viambishi {me} na {ki} vya wakati kadiri ya hali hutumiwa kuelezea hali hiyo.
Tazama jinsi viambishi hivi vinavyojitokeza katika sentensi ifuatayo: Nimekuwa nikimwonya kuhusu madhara ya dawa za kulevya. Katika sentensi hii, neno “nimekuwa” limeundwa kwa muungano wa viambishi {ni} na {me} na kitenzi ( -wa ) cha silabi moja. Kitenzi hiki ambacho tumekitaja mwanzomwanzo mwa makala huleta dhana ya kufanyika au kutendeka.
Matumizi ya {ki} yanapotanguliwa na {me} katika sentensi, sentensi yenyewe huwa haionyeshi wakati maalumu wa kutendeka kwa kitendo ila huonyesha kuwa kitendo kimekuwa kikitendeka kwa muda fulani usiojulikana.
Alhasili, ni kosa kutumia neno shinda kwa maana ya “muda baada ya muda” au “muda mwingi”. Iwapo kitendo kimechukua muda fulani kutendeka au kimekuwa kikirudiwa kila baada ya muda mfupi, viambishi {ki} na {me} hutumiwa kuelezea hali hiyo.