• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
ECO Bank FC yailia njama KCB

ECO Bank FC yailia njama KCB

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya ECO Bank FC inapania kukazana kwa udi na uvumba itakapokabili KCB Alhamisi hii kwenye nusu fainali ya michezo ya kufukuzia taji la Mashirika ya Kifedha (Interbanks) inayoendelea katika uwanja wa KSMS, Nairobi.

Nahodha wa ECO Bank, Edwin Waithera anasema, ”Kusema kweli tunatarajia ushindani mkali mbele ya wapinzani wetu lakini kamwe hatuogopi chochote tumepania kujituma kiume kutafuta tikiti ya kufuzu kushiriki fainali ya mwaka huu.”

Aliongeza kuwa wanafahamu soka haina heshima na chochote kinaweza kutokea licha ya kwamba watacheza dhidi ya wenzao ambao wameshiriki kiwango hicho mara kadhaa. Pia anakiri kuwa patashika hiyo inatazamiwa kuzua msisimko wa kufa.

ECO Bank FC ilitwaa tikiti ya mchezo huo ilipolaza Gulf African Bank FC mabao 2-0 katika robo fainali iliyochezewa uga wa Stima Club, Nairobi.

Kwenye matokeo hayo, KCB ilizoa ufanisi wa mabao 2-1 dhidi ya Consolidated Bank FC iliyoibuka ya pili kwenye kipute hicho mwaka uliyopita. Nayo National Bank of Kenya (NBK) iliangukia pua ilipokubali kuchapwa mabao 2-1 na Equity Bank FC huku Bank of Afrika (BOA) ikitandika Central Bank of Kenya (CBK).

Licha ya Gulf African Bank FC ya kocha, Abdul Aziz kuteremsha soka safi, ilijikuta pabaya ilipokubali kunyukwa na wapinzani hao kupitia mabao yaliyofunika kimiani na Dennis Ndoji.

KCB na Consolidated kila upande ulianza mchezo huo kwa kasi kwenye jitihada za kutafuta mabao ya mapema.

Katika dakika ya 10 KCB ilijiweka kifua mbele ilipopata bao la kwanza lililojazwa kimiani na Rama Chimako kabla ya Consolidated kusawazisha dakika ya 50.

Hata hivyo wachezaji wa KCB waliendelea kukaza buti na kubahatika kutimiza azma ya kusonga mbele kupitia shuti iliyofumwa wavuni na Bethwel Kiplagat dakika 20 baadaye.

”Mechi ilikuwa safi wala siwezi kulaumu waamuzi kabisa lakini vijana wangu walikosa ujanja na kupoteza nafasi chache walizopata huku wapinzani wetu wakitumia vizuri nafasi mbili walizopata,” alisema kocha wa Consolidated Bank, Tobias Ochola.

Equity Bank – mabingwa watetezi – ilitandaza soka safi na kujipatia mabao hayo kupitia juhudi zake Brian Kipkemboi na Derrick Ayisi ambaye ndiye mfungaji bora wa kikosi hicho.

You can share this post!

NLC: Tiya Galgalo atemwa na wabunge

Kioja mzee kupashwa tohara kabla ya kuzikwa

adminleo