TAHARIRI: Wakulima wa majanichai wasipuuzwe
Na MHARIRI
SERIKALI inahitajika ichunguze shutuma zinazotolewa na wakulima dhidi ya Mamlaka ya Ustawi wa Majanichai (KTDA) nchini, kuhusu malipo duni wanayopokea kwa zao lao.
Wakulima wametishia kuacha kukuza majani chai hususan baada ya bonasi ya mwaka huu kupungua kwa kiasi kikubwa zaidi kuliko miaka iliyopita.
Wakulima wanashangaa kwa nini bei hiyo imepungua ilhali hakujakuwa na mtikiso mkubwa katika soko la kimataifa.
Baadhi ya wakulima wameapa kukiuka kanuni za viwanda vyao na kusaka wanunuzi wa kibinafsi angalau wapate faida.
Mwenyekiti wa KTDA Bw Peter Kanyago mapema mwezi huu alitangaza kuwa, bonasi itapungua kuliko iliyolipwa mwaka jana, akisema hiyo imechangiwa na misukosuko katika masoko makuu ya Pakistan, Sudan na Uingereza.
Hakuna mkulima atapokea zaidi ya Sh40 kwa kilo ya majani chai aliyowasilisha kiwandani. Baadhi wataenda nyumbani na Sh10 pekee kwa kila kilo.
Lakini kulingana na mtazamo wa wakulima na viongozi wa maeneo yanayopanda majani chai, utepetevu katika KTDA ndio umefanya hali hii kutokea.
Serikali inafaa kusikiza malalamishi ya wakulima na kuweka mikakati ya kuimarisha KTDA iwapo kweli kuna utepetevu.
Malipo duni hayawezi kulipia pembejeo za kukuza majani mengine na kuna hatari sekta hii inayotegemewa kuletea nchi mapato ya kigeni huenda ikadorora katika miaka ijayo ikiwa suala hili litachukuliwa kwa mzaha.
Aidha, wakulima watakuwa wamefanya kazi bure kuona zao lao linaletea serikali pesa za kigeni lakini wao wanayoyomea katika umaskini. KTDA inafaa kuwakinga wakulima na madhara ya soko la kimataifa. Iko na wataalamu wa kutosha kutathmini hali ya soko mapema na kusaka masoko mbadala.
Vilevile, wakulima wamekuwa wakitaka kuwepo kwa wadau zaidi wa kuuza majani chai badala ya mamlaka moja pekee.
Ni wazo ambalo serikali inafaa kutafakari kwani itaondoa ukiriritimba wa KTDA na kuimarisha ushindani, ambao nao utakuza utendakazi bora na hivyo malipo mazuri kwa wakulima.
Teknolojia pia ni mbinu nyingine ambayo serikali inafaa kuwazia ili kuuza majani chai ya wakulima kwa urahisi.