Habari

Wabunge wailaumu KRA kwa kushindwa kukusanya Sh158 bilioni

September 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

MAMLAKA ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) Jumatano ililaumiwa kwa kufeli kukusanya ushuru unaofikia kiasi cha Sh158 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2014/2015.

Ufichuzi huo uko katika ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ya mwaka huo ambayo ilikuwa ikikaguliwa na Kamati ya Bunge kuhusu Uwekezaji (PIC).

Kamishna Mkuu wa KRA James Mburu ambaye alifika mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir alisema kufikia sasa mamlaka hiyo imekusanya Sh112 milioni kati ya fedha hizo ambazo zimejilimbikiza kwa miaka minne.

“Hicho ni kiwango kikubwa cha fedha. Ikiwa kufikia Juni 30, mwaka huo KRA ilikuwa haijakusanya Sh158 bilioni inamaanisha kuwa kiasi hicho cha pesa kimeongezeka sasa,” akasema Bw Nassir.

Hata hivyo, Bw Mburu aliwaambia wabunge hao kwamba KRA sasa imeweka mikakati murwa ya kuimarisha kiwango cha ukusanyaji ushuru mwingi.

“Tutahakikisha kuwa kila mtu analipa ushuru kama inavyohitajika kisheria kupitia mikakati ambayo tumeweka,” akasema kamishna huyo mkuu.

Bw Mburu aliwataja wafanyakazi kadha ambao wameshtakiwa kwa kukwepa kulipa mabilioni ya fedha kama ushuru, ishara ya kujitolea kwa KRA kukusanya ushuru zaidi.

Baadhi ya wafanyabiashara ambao hivi majuzi walikamatwa kwa madai ya kukwepa kulipa ushuru ni Bi Tabitha Karanja na Bw Joseph Karanja ambao ni wakurugenzi wa kampuni ya kutengeneza pombe na mvinyo ya Keroche Breweries Limited.

Naye mfanyabiashara Humprey Kariuki, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya kutengeneza mvinyo ya African Spirits amekanusha mashtaka ya kukwepa ulipaji ushuru unaofikia zaidi ya Sh17 bilioni.