Raila akosa kufaulu kumtimua Chebukati na wenzake wawili
Na CHARLES WASONGA
MPANGO wa kiongozi wa ODM Raila Odinga wa kutaka mwenyekiti wa Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati na makamishna wawili waondolewe mamlakani kabla ya muhula wao ulifeli Jumanne jioni.
Hii ni baada ya wabunge wandani wa Naibu Rais William Ruto kuungana na kupitisha mswada wa marekebisho ya sheria ya IEBC inayopendekeza kuundwa kwa jopo la kujaza nafasi ya zitakazosalia wazi katika tume hiyo.
Lakini wabunge walioegemea upande wa Bw Odinga walipinga kipengee katika mswada huo kinachosema makamishna walioko sasa watasalia afisini na kwamba nafasi zilizo wazi ndizo zitajazwa.
Bw Odinga amekuwa akitaka Bw Chebukati na makamishna Boya Molu na Abdi Guliye watimuliwe na vyama vya kisiasa vinavyowakilishwa bungeni vipendekeze majina ya watu wapya watakaochukua nyadhifa hizo.
Kati ya wabunge 126 waliokuwa bunge siku hiyo, 69 waliunga mkono mswada huo huku 56 wakiupinga.
Wale waliunga mkono mswada huo uliodhaminiwa na Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) ni wale wanaounga mkono azma ya Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022. Kamati hiyo inaongozwa na Mbunge wa Baringo Kaskazini William Cheptumo.
Baadhi yao ni kiongozi wa wengi Aden Duale, Rachael Nyamai (Kitui Kusini), Didmus Barasa (Kimilili), Joseph Limo (Kipkelion Mashariki), Julius Meli (Tinderet), Jude Njomo (Kiambu), John Kiarie (Dagoretti Kusini) miongoni mwa wengine.
Na waliopinga mswada huo ni pamoja na kiranja wa wachache Junet Mohamed, Wilson Sossion (Mbunge Maalum) Gathoni Wa Muchomba (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kiambu katika Bunge la Kitaifa), William Kamket (Tiaty), Jared Okello miongoni mwa wengine.
Kujaza nafasi
Endapo Rais Uhuru Kenyatta atautia saini mswada huo kuwa sheria, jopo la watu 11 litateuliwa kujaza nafasi ya makamishna wanne waliojiondoa.
Wao ni Dkt Roseline Akombe, Consolata Bocha Maina, Dkt Paul Kurgat na Bi Margaret Mwachanya Wanjala.
Dkt Akombe alijiuzulu mnamo Oktoba 20, 2017, kabla ya marudio ya uchaguzi wa urais na huku wengine wakijiondoa Aprili 20, mwaka jana.
Bw Odinga na wafuasi wake wamekuwa wakishinikiza Bw Chebukati na wenzake wafutwe kazi kwa kuendesha visivyo uchaguzi wa 2017 haswa ule wa urais.