Msajili akataa Tangatanga, Kieleweke
Na LEONARD ONYANGO
JUHUDI za baadhi ya wanasiasa kutaka kugeuza makundi ya ‘Kieleweke’ na ‘Tangatanga’ kuwa vyama vya kisiasa zimegonga mwamba, baada ya Msajili wa Vyama, Bi Ann Nderitu kuzuia majaribio hayo yaliyofanywa zaidi ya mara mbili.
Vilevile, Bi Nderitu alisema kuna kundi jingine lililotaka kusajili ‘Handshake’ kuwa chama cha kisiasa lakini pia jaribio hilo likatibuliwa.
Imebainika Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa imepokea maombi mara nne ya kutaka Tangatanga Movement kisajiliwe kuwa chama, na ombi la Kieleweke kutumwa kwa ofisi hiyo mara tatu.
Ombi la kwanza la kutaka Tangatanga Movement kusajiliwa kuwa chama liliwasilishwa mara tu baada ya makundi mawili; Tangatanga na Kieleweke kujitokeza katika chama cha Jubilee mwaka 2018, kulingana na Bi Nderitu.
Jaribio la mwisho lilikuwa wiki iliyopita ambapo makundi mawili yalimwandikia barua Bi Nderitu yakimtaka asajili Tangatanga Movement (TTM) na Mafisi Alliance Party (MAP) kuwa vyama vya kisiasa.
Lakini Bi Nderitu, alikataa kusajili Tangatanga na Mafisi akisema majina hayo yanakiuka Katiba na Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2011.
“Majina Tangatanga, Mafisi yanakiuka maadili na yanakiuka Kifungu cha 91 cha Katiba. Tafadhali pendekeza majina mengine ili tuyachunguze,” Bi Nderitu akayaeleza makundi hayo.
Msajili wa vyama hivyo pia alitoa sababu sawa na hiyo alipokataa kusajili Kieleweke Movement kuwa chama.
Kundi la Tangatanga linaunga mkono Naibu wa Rais William Ruto huku Kieleweke likiunga mkono mwafaka (handisheki) wa kisiasa baina ya Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga.
Hata hivyo haijulikani ikiwa makundi yaliyojaribu kusajili Tangatanga, Kieleweke au ‘Handshake’ yanafanya hivyo kwa niaba ya Dkt Ruto, Rais Kenyatta au Bw Odinga.
“Maombi ya kutaka kusajili vyama mara nyingi huwasilishwa na mawakili hivyo ni vigumu kujua mtu aliyewatuma,” akasema Bi Nderitu kwenye mahojiano na Taifa Leo.
Aibu
Kulingana na Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2011, Msajili wa vyama anaweza kukataa kusajili chama ikiwa jina lake linaleta aibu au matusi, linafanana na vyama ambavyo tayari vimesajiliwa au nembo yake ni sawa na ya vyama vilivyopo.
“Ombi la hivi karibuni la kutaka Handshake Alliance kisajiliwe kuwa chama liliwasilishwa Jumatano, wiki hii, lakini nikakataa kukisajili. Makundi yaliyowasilisha maombi hayo hayakutimiza matakwa ya sheria,” akasema Bi Nderitu.
Kifungu cha 91 cha Katiba kinasema chama hakitasajiliwa ikiwa kimebuniwa kwa misingi ya dini, kabila, jinsia, vurugu au uchochezi.
“Chama cha kisiasa ni sharti kiwe na sura ya kitaifa, kionyeshe umoja wa nchi na kionyeshe maadili,” inasema Katiba.
Vyama vya kisiasa vilivyosajiliwa kuendesha shughuli za kisiasa nchini ni 68.
Vyama ambavyo vimetuma maombi lakini havijaidhinishwa kujihusisha na siasa ni 37, kulingana na Msajili wa Vyama vya Kisiasa.
Miongoni mwa vyama vinavyongojea kuidhinishwa ni Wema Wetu, Undugu Unity, Mwamba Wetu Social Party, Miradi People’s Socialist, Ajibika For Change Party, Haki na Utaifa Party kati ya vinginevyo.