Michezo

Kenya yaendelea kuumia mashindano ya voliboli

September 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

KENYA itajilaumu yenyewe kwa kutoshinda hata seti moja kufikia sasa katika Kombe la Dunia la voliboli ya wanawake baada ya kupokea kichapo chake cha tisa kwa kubwagwa 3-0 na Korea Kusini mjini Sapporo nchini Japan, Ijumaa.

Malkia Strikers ilizidiwa maarifa na Wakorea katika seti mbili za kwanza hasa katika upokeaji wa mipira na kuzipoteza kwa alama 25-15 na 25-16, mtawalia.

Hata hivyo, vipusa wa kocha Paul Bitok waliimarika katika seti ya tatu baada ya kurekebisha kosa hilo.

Waliongoza Korea Kusini hadi alama 20-18 waliporudia kosa na kushuhudia wakifungwa alama saba bila jibu na kupoteza nafasi hiyo ya kushinda seti moja.

Mabingwa hao wa michezo ya Afrika waliingia mechi ya Korea Kusini wakiuguza vipigo vya seti 3-0 kutoka kwa Marekani (Septemba 14), Uholanzi (Septemba 15), Serbia (Septemba 16), Brazil (Septemba 18), Argentina (Septemba 19), Jamhuri ya Dominican (Septemba 22), Japan (Septemba 23) na Uchina (Septemba 24).

Baada ya kucheza dhidi ya Korea Kusini, Bitok alisema, “Katika seti mbili za kwanza, ilikuwa vigumu kwetu kucheza kwa sababu upokeaji wetu wa mipira ya pembeni ulisambaratika. Tulijaribu kurekebisha kosa hili katika seti ya tatu na ikafanya kazi vyema hadi tuliporudia kosa baada ya kufika alama 20. Hii iliruhusu Korea kufunga alama saba mfululizo kutoka 18 hadi 25. Natumai hatutarudia kosa hili tena katika mechi zijazo. Lengo letu ni kubwaga Cameroon (katika mechi yetu ya mwisho hapo Septemba 29), ingawa kwa sasa akili zetu ziko katika kupambana na Urusi hapo Jumamosi. Tunataka kuimarika tunapokutana na timu kubwa.”

Nahodha wa Kenya, Mercy Moim alikiri walipoteza mwelekeo baada ya kuanza vizuri katika seti ya tatu.

“Mechi haikuwa nzuri wala mbaya. Katika seti mbili za kwanza, tulicheza vibaya na kuruhusu Korea kutumia silaha zake kali. Katika seti ya tatu, tulianza vyema, lakini tukamaliza vibaya kwa hivyo tukapoteza seti hiyo. Kesho, tutakutana na Urusi na tutashughulikia idara yetu ya kupokea mipira na pia ulinzi kwa sababu tunatatizika sana katika idara hizi. Urusi haichezi mchezo wa kasi ya juu kama Korea kwa hivyo tutafanyia kazi uzuiaji wetu wa mipira, kupokea mipira na pia ulinzi.”