Makala

MUTUA: Hadhi yetu isidhalilishwe kimataifa na wanaopora

September 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na DOUGLAS MUTUA

MOJAWAPO ya matusi maarufu zaidi dhidi ya raia wa kigeni nchini Rwanda humkanya mtu kutofanya mambo polepole kama Mtanzania.

Nalo tusi maarufu zaidi dhidi ya wageni nchini Tanzania ni kwamba, usiwe mwizi kama Mkenya.

Anayekutukana hakuchagulii tusi, hivyo kuyatilia maanani sana ni sawa na kumsaidia anayeyatema kuendeleza chuki na ubaguzi.

Bila shaka, matusi kama hayo si mzaha kwa maana hayatokani na mapenzi bali chuki ya jumla dhidi ya walengwa. Yanasikitisha.

Hata hivyo, ukizingatia kwamba kila jamii tangu hapo ikijituma kujilinda dhidi ya kukaliwa kimabavu na jamii au nchi nyingine yoyote, yanaeleweka.

Tatizo linaingia matusi yenyewe yanaporudiwa sana kiasi cha kumfanya mlengwa kuyaamini na kuanza kuenenda kama matusi yenyewe yanavyoashiria.

Kwa wakati huu, sitaki kujadili kasi au mwendo wa pole wa Mtanzania.

Hata hivyo, sitaisaza nchi yangu Kenya. Haidhuru kumjadili mbaya wako kwa madhumuni ya kumrekebisha. Kenya, taifa lenye nguvu zaidi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, limekuwa kivutio cha wengi kwa muda mrefu kutokana na maendeleo na ujasiriamali wetu.

Wakati mmoja, mwanzilishi wa taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kuajabia maendeleo ya Kenya, aliwashauri Watanzania wakitaka kuzuru jiji la kisasa waje Nairobi, wasiende London.

Japo sisi wenyewe tumekuwa na matatizo yetu ya kisiasa na utovu wa usalama, tumepiga hatua kadhaa na kurejesha imani ya wengi kuhusu uthabiti wetu.

Ndiyo maana unawaona wakimbizi wakimiminika huku kila kunapotokea ghasia kokote Afrika Mashariki na Kati.

Kwa muda mrefu, Kenya imewahifadhi raia wa Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC); Ethiopia, Somalia na kadhalika.

Hata tusipokuwa na ujirani mwema, ni hulka ya binadamu kumtendea wema anayekumbwa na misukosuko ya kimaisha. Umoja wa Mataifa (U.N.) unaagiza hivyo.

Wasomi wa Kenya wametapakaa kila mahali Afrika na duniani ambako wanafanya kazi mbalimbali, kuu zaidi zikiwa kugawa maarifa kwa njia ya kudundisha.

Afrika, utawapata Rwanda, Burundi na Sudan wakifundisha Kiswahili, ukiteremka kidogo uwapate Botswana na Afrika Kusini wakifundisha vyuo vikuu.

Pia utawapata Watanzania, hasa kwenye shule binafsi, wakifundisha Kiingereza, Hisabati na masomo mengine mengi.

Ingawa Tanzania ingetaka kutusadikisha kwamba Kiswahili kinazungumzwa zaidi nchini humo, utaalamu wa kukifundisha ni milki ya Wakenya.

Idadi ya walimu wa Kiswahili kote duniani inaizidi sana ile ya Watanzania. Si siri. Bila shaka tumesaidiwa sana na uelewa wetu wa Kiingereza. Watanzania wanakijaribisha tu.

Hata hivyo, kuna tatizo kubwa. Maarifa yote tuliyonayo yanaweza kukosa tija yoyote ikiwa tusi la Watanzania kwamba sisi ni wezi litatokea kuwa kweli au liaminike kote barani.

Nchi ikipata aibu kiasi hiki inaelekea pabaya. Ikiwa huniamini, niambie kwa nini unaingia baridi unapojipata ukitekeleza muamala wa kifedha na raia wa Nigeria. Hao nao jina lao limeoza! Ni sharti tujirudi kabla ya dunia kutukataa.

 

[email protected]