• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
UMBEA: Iwapo hakupendi mpishe na umpatie nafasi, usijaribu kulazimisha mambo!

UMBEA: Iwapo hakupendi mpishe na umpatie nafasi, usijaribu kulazimisha mambo!

Na SIZARINA HAMISI

KATIKA pitapita zangu hivi karibuni, nilikutana na dada ambaye alinisimulia mengi kuhusu ndoa yake.

Akanieleza jinsi anavyotatizika na maisha ya ndoa na kwamba anaishi na mumewe sababu hana kazi na pia sababu mume ndiye anayemtimizia mahitaji yake yote.

Akanidokeza zaidi kwamba iwapo atapata kazi na kuweza kujimudu kimaisha, basi nia yake ni kuondoka na kuanza maisha yake binafsi.

Nilipomwuliza ameishi katika hali hiyo kwa muda gani, akanieleza kuwa ni zaidi ya miaka mitano ambayo amekuwa na mumewe.

Akanieleza zaidi kwamba mumewe ana tabia zilizopinda na amekuwa anamnyanyasa na kumtesa, lakini imebidi aishi naye sababu ya uwezo wake kimaisha. Jambo kubwa zaidi ya yote, huyu dada akanieleza kwamba hampendi mumewe na wala hana tena mvuto naye hata chembe.

Katika maelezo yote aliyonipa, tathmini yangu ya awali ni kwamba huyu dada anaishi katika utumwa wa mapenzi. Kwamba anaishi na mumewe, hana mapenzi naye, lakini inambidi aendelee kuishi naye kwa sababu ya maslahi binafsi.

Unakuta mwanamke anaamua kuwa na mwanaume fulani ingawa anajua wazi kwamba hampendi lakini kwa sababu jamaa keshaonyesha mapenzi kwake na anajua wazi anampenda, basi anakubali kwa sababu ya kupata kitu.

Wapo wanaokuwa na uhusiano na wapenzi ambao hawana kabisa mapenzi nao. Wanalazimika kuwa nao kwa sababu mbalimbali, mojawapo ikiwa ni kupenda kupita kiasi huku wakitumia ushawishi wa kila aina ili nao wapendwe.

Wanafanya hivyo kwa sababu wanafahamu wazi kwamba hawapendwi.

Wakati mwingine ni kutokana na shinikizo la ndugu, jamaa au marafiki, kumshawishi aendelee kung’ang’ania mahali kwa sababu ya maslahi ama labda sababu ya kukidhi matakwa ya jamii.

Iwapo upo katika tafrani hii, utambue kwamba ni kazi ngumu mno kumbadilisha binadamu mwenzako, iwapo hakupendi mpishe na umpatie nafasi, usilazimishe mambo.

Huna haja ya kuunyima moyo wako haki ya kuwa na yule unayempenda zaidi, mapenzi hayalazimishwi. Fedha, mali na anasa zote hutafutwa na hata siku moja haziwezi kununua penzi la dhati. Anza kubadilika, ondoa fikra zako mgando na uingize ufahamu mpya utakaokuweka katika ramani ya maisha ya kibinadamu na siyo ya kinyama kama uliyo nayo sasa.

Ujumbe wa leo pia ni kwa wazazi ambao wanachochea mabinti zao waishi na wanaume wasiowapenda na kuwatumia kama chanzo cha kipato. Kwani shinikizo hili hupelekea watoto kujipata wakiishi katika ndoa ambazo zinafanana na gereza la mapenzi.

Yakishamwagika hayazoleki

Siku zote, maji yakishamwagika hayazoleki. Kwa wale ambao tayari wameshafunga ndoa, inakuwa ni vigumu kuvunja muunganiko huo na hivyo watajikuta wakiendelea kuteseka badala ya kufurahia maisha ya ndoa ama mahusiano.

Na hali hii ikiendelea kwa muda mrefu, ndiposa mmoja anaweza kuamua kutafuta pumziko nje ya ndoa yake na matokeo yake yakawa ni kuleta sokomoko na mshike mshike.

Iwapo ni mzazi, mpatie nafasi mwanao ya kumchagua yule anayemtaka, akiwa ni mwenye pesa ni sawa na akiwa ni kuli mbeba mizigo bandarini, pia ni sawa. Nafasi yako kama mzazi ni kumshauri mwanao iwapo utaona anakuwa katika uhusiano ambao una mashaka nao.

Kumng’ang’aniza mwanao kuwa katika uhusiano ambao yeye haupendi ni kumharibia maisha yake, maana badala ya kufikiria maisha yake, atajikuta akifikiria jinsi alivyo katika gereza la watumwa wa mapenzi. Mpatie nafasi mwanao aishi maisha yale aliyojichagulia na sio uliyomchagulia.

Wazazi badilikeni!

 

[email protected]

You can share this post!

MWANAMUME KAMILI: Jamani wazazi pimeni semi kabla kutamka!

FATAKI: Mwanamume ni nguzo kuu katika maisha ya wanawake

adminleo