Makala

FATAKI: Mwanamume ni nguzo kuu katika maisha ya wanawake

September 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

KUNA msemo maarufu wa Kiingereza ‘behind every successful man, there’s a woman’, unaotambua mchango wa wanawake katika ufanisi wa wanaume.

Na ni kweli kabisa. Lakini hata tunavyosema hivi, kuna jambo ambalo jamii imesahau kabisa. Kwamba wanaume wamechangia pakubwa katika ufanisi wa wanawake; yaani ukichunguza vyema wanawake waliobobea katika nyanja mbalimbali, utagundua kwamba walipata kivuli chini ya ubavu wa mwanamume fulani.

Yaweza kuwa ni baba, ndugu, mfanyakazi mwenza, rafiki wa karibu, mume, mpenzi au hata baba sukari.

Ndiposa katika jamii yoyote iliyo na ufanisi, utapata kwamba wanaume pale wamewahimili vilivyo mabinti, dada au wake zao, hivyo kuwasaidia kuinuka.

Si eti nawapigia debe ila kuna mifano thabiti kuashiria nisemayo. Tuchukue mfano wa magwiji wa tenisi Serena na dadake Venus Williams. Baba yao, Richard Williams ndiye alitambua vipaji vyao na akaanza kuwapiga nakshi kama mkufunzi wao. Aliwathibitishia uwezo wao na kuwasaidia kupaa juu ya vikwazo kama vile ubaguzi wa rangi.

Mfano mwingine ni mwanamuziki Beyonce. Haina shaka kwamba Mathew Knowles alichangia pakubwa ustawi wake kimuziki. Beyonce amewahi kukiri kwamba babake alimfunza kuwa mkakamavu, mojawapo ya mawaidha yaliyomsaidia kupaa katika ulingo wa muziki.

Mifano sawa na hiyo pia iko hapa nchini.

Kwa mfano, ufanisi wa bilionea Tabitha Karanja, mumliki wa kampuni ya mvinyo na pombe ya Keroche Breweries Limited, ulichangiwa pakubwa na mumewe Joseph Karanja ambaye ndiye aliyefungua biashara hiyo kabla ya kumshawishi mkewe kuungana naye.

Mwanamke wa kwanza wa Kiafrika kusomea Chuo Kikuu cha Harvard nchini Amerika, na mtaalamu wa masuala ya lishe nchini, Julia Ojiambo, pia amenukuliwa mara kadha wa kadha akimsifia marehemu mumewe kama nguzo kuu ya ufanisi wake.

Sio hawa tu. Orodha hii ni ndefu na nafasi niliyonayo haitoshi. Lakini ujumbe ninaopitisha ni kwamba, japo pia kumekuwa na hadithi za wanaume ambao wamekuwa vizingiti kwa ufanisi wa wanawake, vilevile idadi kubwa imechangia kuinuka kwa wanawake na hivyo hawawezi kupuuzwa.

Hatukatai kwamba wanawake wanaweza ila tutakuwa tunadanganyana kudhani kwamba katika safari hii ya usawa wa kijinsia, watafanikiwa pasipo kuwahusisha wanaume.