• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 7:55 AM
DAU LA MAISHA: Awafanyia ukarimu chokoraa mtaani

DAU LA MAISHA: Awafanyia ukarimu chokoraa mtaani

Na PAULINE ONGAJI

KWA miaka minne sasa amejitwika jukumu la kusaidia watoto wanaorandaranda mitaani.

Devian Kwamboka ameifanya kazi hii tangu mwaka wa 2015 kupitia mradi alioanzisha wa Out of The Street Organization, chini ya kauli mbiu ‘kutoa mtoto kwenye street’.

Shirika hili lenye makao yake katika kitongoji duni cha Majengo viungani mwa jiji la Nairobi, limekuwa likiendesha shughuli katika ukumbi wa kijamii mtaani humo, lakini mara nyingi huwatembelea vijana hawa katika sehemu ambapo wamekita kambi.

Aidha hutekeleza haya kupitia sanaa ambapo miradi yao imegawanywa katika sehemu nne.

Sehemu ya kwanza ni uundaji kuchakata plastiki na vitambaa ili kuunda bidhaa za mapambo.

“Kwa mfano sisi huunda vifuasi vya kimapambo kwa kutumia plastiki na vitambaa vya Ankara,” aeleza.

Kitengo cha pili kinahusisha urekebishaji tabia kuwanasua kutokana na matumizi ya mihadarati.

Kisha sehemu ya tatu inashughulikia afya njema ambapo wamekuwa wakiandaa kambi za kimatibabu kwa ushirikiano na washirika wao katika sekta ya afya.

Bi Devian Kwamboka, mwanzilishi wa Out of The Street Organization, shirika linalosaidia vijana wanaorandaranda mitaani kupata hifadhi. Picha/ Evans Habil

Nguzo yao ya nne ni elimu ambapo kuambatana na azimio la nne la maendeleo endelevu (SDG 4) la usawa katika elimu, wako katika harakati za kujenga maktaba ya kijamii katika kitongoji duni hiki.

“Tayari tumefanya kampeni za kukusanya vitabu kadha. Lakini bado tunahitaji usaidizi zaidi ambapo mambo yakienda vyema, tutazindua maktaba hii mwezi ujao,” aeleza.

Mara nyingi ufadhili wao unatokana na wahudumu wa kujitolea.

“Tuna wahudumu 50 wa kujitolea ambao hutusaidia kuelimisha vijana kuhusu masuala ya matumizi ya mihadarati, vile vile athari za kujihusisha na ngono mapema,” aeleza.

Aidha, tuna washirika wengi hasa katika nyanja ya afya na mara nyingi hutusaidia tunapoandaa kambi za kiafya.

Na mradi huu umekuwa na matokeo mazuri kwa jamii ambapo kufikia sasa watoto watano wameokolewa kutoka mitaani na wanajiendeleza kimaisha.

“Watano hawa wana kipaji cha kucheza densi. Tuliwatambua kupitia kambi zetu, kisha tukawaunganisha na kuwa kikundi na sasa wameweza kuondoka mitaani. Kupitia vipaji vyao, wamekuwa wakifanya shoo na kupata hela kidogo za matumizi,” aeleza.

Vile vile, wameweza kuandaa kambi tano za kiafya, na hivyo kusaidia wakazi wa mtaa huu kupokea huduma za kimatibabu.

“Kwa mfano mwaka 2019 tuliandaa kambi ambapo zaidi ya wakazi 2000 walinufaika,” asema.

Mbali na hayo, Bi Kwamboka anasema kwamba mradi huu umemfunza mengi kwani umemhimiza kutafuta taarifa zaidi kuhusu elimu na usimamizi wa kijamii.

Hamu

Bi Kwamboka alianza shughuli hii mwaka wa 2015 huku akichochewa na uchu wa kutaka kuona watoto hawa wakiishi maisha ya kawaida.

“Niliona haja ya kuwasaidia kwani nilihisi kwamba kungewapa fursa maishani katika siku za usoni.

Licha ya kuwa hanufaiki kwa vyovyote kutokana na kazi anayofanya, anakaza kamba kwani anaona ni kama njia ya kuhudumia jamii. “Ni mradi ambao kila siku unanikumbusha jinsi nilivyobahatika maishani mwangu kwani mambo ninayoyachukulia kuwa ya kawaida, wengine hawawezi kuyapata,” aeleza.

Huku akitumai kuendeleza mradi huu katika sehemu zingine nchini, Bi Kwamboka ambaye aliwahi kushiriki katika mradi wa uongozi wa YALI (Young African Leaders Initiative), amejiandikisha kozi za mtandaoni katika Chuo Kikuu cha Michigan nchini Amerika, kusomea masuala ya usimuliaji hadithi kuleta mabadiliko katika jamii.

You can share this post!

FATAKI: Mwanamume ni nguzo kuu katika maisha ya wanawake

SHANGAZI AKUJIBU: Anataka kunioa ila SMS za wapenzi wake...

adminleo