• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
‘Malkia Strikers yaimarika pakubwa licha ya msururu wa matokeo mabaya’

‘Malkia Strikers yaimarika pakubwa licha ya msururu wa matokeo mabaya’

Na GEOFFREY ANENE

KAMBI ya Kenya imefurahia mchezo wake licha ya Malkia Strikers kupoteza mechi yake ya 10 mfululizo kwenye Kombe la Dunia bila kupata seti ilipochapwa na mabingwa wa mwaka 1973 Urusi nchini Japan, Jumamosi.

Warembo wa kocha Paul Bitok waliandikisha alama 25-16, 25-21, 25-22 katika seti hizo uwanjani Edion mjini Osaka.

Baada ya mechi hiyo, Bitok alisema, “Nataka kupongeza rafiki yangu na kocha (Sergio Busato) kwa kuwa na mashindano mazuri katika kombe hili. Kivyangu, nafurahia mchezo wa timu yangu. Mwanzoni mwa mashindano haya, nilijiambia kuwa nataka kufanya vitu ambavyo miamba ya voliboli ya wanawake inafanya. Tumeanza kucheza kama miamba. Hatujaweza kudhibiti mchezo wetu, lakini tumeanza kuwa na mchezo ulio na kasi. Tunatumia mbinu fulani katika kuzuia mashambulizi na katika mashambulizi yetu, lazima tuongeze kasi yetu ili tufanikiwe kuundia washambuliaji wetu nafasi. Natumai wachezaji hawa wamejifunza na nimesisitiza tuendelee na mfumo huo. Tunaweza kushinda ama tusishinde, lakini unavyoona, kile tumeanzisha kimeanza kuzaa matunda. Mara nyingi, hatukuweza kufikisha alama 10 dhidi ya Urusi, lakini leo tulifika 21, 22. Haya ni mafanikio makubwa kwetu. Najua kila mtu anatarajia tushinde seti kadhaa, lakini nilivyosema tunaanza kucheza voliboli ya kisasa na katika miaka miwili ama mitatu, tunaweza kuwa bora zaidi. Ijumaa, tulitatizika katika kupokea mipira. Tulishughulikia idara hii mapema Jumamosi na leo tulikuwa asilimia 70 bora. Nilivyosema, bado hatujaweza kudumisha mchezo wetu, lakini ni kwa sababu mbinu hizi bado ni mpya kwetu. Naamini zinafanya kazi vyema. Natumai hatutalegeza kamba dhidi ya dada zetu kutoka Afrika, Cameroon, na naamini tukikutana na Urusi tena, tutanyakua seti kadhaa. Tulikutana na Cameroon mara mbili mwezi Agosti na tukashinda mechi moja na kulemewa nyingine. Tunataka kushinda Jumapili ili tujue tumefika wapi kimchezo kabla ya kukutana nao tena katika mechi za kufuzu kushiriki Olimpiki. Itatufanya tujiamini zaidi na pia wachezaji kujiamini tutakuwa na nafasi nzuri tukirejea hapa nchini Japan mwaka 2020.”

Nahodha aridhishwa

Nahodha wa Kenya, Mercy Moim pia aliridhishwa na jinsi Malkia Strikers ilicheza.

“Leo, tulicheza mechi nzuri. Urusi ni timu kubwa na kufikisha alama 21 na 22 dhidi yao ni mafanikio makubwa kwa timu yangu. Ijumaa, niliwaeleza kuwa tutafanyia kazi idara zetu za kupokea mipira na ulinzi na hivyo ndivyo tulifanya, na unaona ilitusaidia sana leo. Jumapili, tunataka kufanya kama Jumamosi kuhusu kuanzisha mipira na kupokea mipira. Sisi hukutana na Cameroon mara nyingi kwa hivyo tunajua nguvu zao pamoja na udhaifu wao,” akasema Moim.

Kocha wa Urusi, Busato pia alikiri aliona Kenya tofauti Jumamosi.

“Kenya ilikuwa na mashambulizi mazuri leo (Jumamosi) na kuanzisha mipira vyema. Naheshimu sana voliboli yao,” akasema Busato.

Kombe hili lilianza Septemba 14. Litakamilika Septemba 29.

You can share this post!

Kuteuliwa kwa Kambi katika NLC kwakoroga baadhi ya wabunge

Polo alilia mke aliyemzaba kofi

adminleo