Habari Mseto

Kuteuliwa kwa Kambi katika NLC kwakoroga baadhi ya wabunge

September 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA na SAMUEL BAYA

UTEUZI wa aliyekuwa Waziri wa Leba Kazungu Kambi kuwa kamishna wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) umeendelea kuibua hisia mseto miongoni mwa wabunge wa pwani huku ukipingwa na muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini (COTU).

Japo uteuzi wa Bw Kambi uliidhinishwa na wanachama wengi wa kamati ya bunge kuhusu ardhi, wabunge watatu kutoka Pwani wamepinga wakidai hajatimiza hitaji la kikatiba kuhusu maadili na maongozi bora.

Lakini Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa amejitokeza kumtetea akisema Bw Kambi anafaa kupewa nafasi ya kuhudumu katika NLC “kwa sababu hajapatikana na hatia kuhusiana na kesi inayomkabili.”

Wabunge wanaopinga uteuzi wa Bw Kambi ni; Mabw Owen Bay (Kilifi Kaskazini), Teddy Mwambire (Ganze) na Omar Mwinyi (Changamwe).

Wanadai kuwa Waziri huyo wa zamani wa Leba anakabiliwa na kesi mahakamani kwa kosa la kutumia cheti cha umiliki wa ardhi ya eneo la Giriama kuchukua mkopo wa Sh250 milioni kutoka benki kupitia kampuni yake kwa jina, Riva Oils.

“Tunataka bunge lipinge uteuzi wa Kazungu Kambi kwa sababu hajatimiza mahitaji ya Sura ya Sita ya Katiba kuhusu Maadili na Uongozi Bora. Vile vile, hajahitimu kimasomo kwa wadhifa huo. Kwa hivyo, tunamtaka Rais Uhuru Kenyatta kuteua mtu mwingine kutoka pwani kwa wadhifa huo,” Bw Baya akasema.

Bw Baya, Bw Mwambire na Bw Mwinyi ambao ni wanachama wa kamati hiyo ya ardhi wameandaa ripoti ya kupinga uteuzi wa Bw Kambi ambayo watawasilisha bungeni Jumanne.

Kesi

Lakini Bi Jumwa anapinga msimamo wa wabunge hawa akisema licha ya kwamba Bw Kambi anakabiliwa na kesi mahakamani, hilo haliwezi kumzuia kuendelea kuhudumia Wakenya akisema endapo atapatikana na hatia atalazimika kujiondoa.

“Hii ndio fursa ya pekee ambayo Rais alitutunuku jamii ya Wamijikenda na tunafaa kuchukulia kwa uzito badala ya kumshambulia mmoja wetu. Sitanyamaza ila nitaendelea kupigania haki za watu wetu. Nitakuwa mtu wa mwisho kupinga mmoja wetu,” akasema Bi Jumwa.

Mbunge huyo alisema ni kinaya kwamba wabunge wa Pwani wamekuwa wakiongea kuhusu umoja wa Pwani lakini sasa baadhi yao wako mbioni kumpiga vita mmoja asipate wadhifa wa umma.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Cotu Francis Atwoli kupitia kwa taarifa kwa vyombo vya habari, anadai Bw Kambi hafai kuidhinishwa kwa wadhifa huo kwa sababu “amepotoka kimaadili.”