MWANASIASA NGANGARI: Achieng Oneko, shujaa aliyetetea ukombozi kwa kinywa kipana

Na KYEB

MPIGANIAJI uhuru Ramogi Achieng Oneko atakumbukwa kwa kuwa mwanasiasa mwenye msimamo thabiti, aliyekuwa tayari kufa akiitetea Kenya.

Ndiye mpiganiaji uhuru pekee aliyefungwa gerezani na serikali ya kikoloni na ile ya Mzee Jomo Kenyatta.

Alikuwa miongoni mwa watu walioteuliwa katika baraza la kwanza la mawaziri na Mzee Kenyatta mnamo 1963. Aliteuliwa kuwa Waziri wa Habari na Utangazaji.

Bw Oneko alizaliwa katika kijiji cha Tieng’a, eneo la Uyoma, Bondo mnamo 1920.

Alipata kazi yake ya kwanza kama ripota wa masuala ya hali ya hewa katika Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa mara tu, baada ya kumaliza masomo yake katika Shule ya Upili ya Maseno.

Alifanya kazi chini ya usimamizi wa Mwingereza ambaye hakumpenda.

Mnamo 1949, alijitosa kwenye siasa, ambapo alichaguliwa kuwa miongoni mwa madiwani wa kwanza Waafrika katika manispaa ya Nairobi.

Oneko vile vile alikuwa miongoni mwa Wakenya wa kwanza kuanzisha gazeti la lugha ya Kiluo liitwalo ‘Ramogi Weekly’ mnamo 1945. Lengo kuu la gazeti hilo lilikuwa kuishinikiza serikali ya kikoloni kuwapa uhuru Waafrika.

Alipata uungwaji mkono kutoka kwa mchapishaji wa Kihindi, G.L. Vidyathi aliyehudumu jijini Nairobi.

Gazeti la pekee la kila siku wakati huo ‘East African Standard’ lilikuwa likiendeleza matakwa ya walowezi wa Kiingereza na maslahi yao.

Oneko vile vile ndiye alikuwa katibu wa chama cha Luo Thrift and Trading Corporation (LTTC) kilichobuniwa na Bw Oginga Odinga, ambaye alikuwa rafiki wake wa karibu. Alihudumu kwenye wadhifa huo kati ya 1948 na 1951.

Bw Oneko alikutana na Mzee Kenyatta katika miaka ya arobaini, alipomhoji kwenye gazeti lake.

Wakati huo, Mzee Kenyatta alikuwa kiongozi wa chama cha Kenya African Union (KAU). Wawili hao waliibukia kuwa marafiki wakubwa, ambapo baadaye, walikamatwa pamoja. Pamoja na watu wengine wanne; Fred Kubai, Kung’u Karumba, Bildad Kaggia na Paul Ngei, waliwekwa kizuizini kwa kuwa wanachama wa Mau Mau.

Oneko ndiye alikuwa mshirika wa karibu zaidi wa Mzee Kenyatta wakati kesi yao ilikuwa ikiendelea katika gereza la Kapenguria. Mahakama haikumpata na hatia, lakini alikamatwa tena na kuwekwa kizuizini akiwa na Mzee Kenyatta na wenzao wanne katika eneo la Lokitaung. Walipewa msimbo wa “Kapenguria Sita.”

Kulingana naye, serikali ya kikoloni iliamini kwamba alikuwa na uhusiano mkubwa na Mzee Kenyatta. Alimtaja Mzee Kenyatta kuwa msomi na mzungumzaji mahiri aliyehutubu kwa ufasaha mkubwa sana wa lugha.

Kutokana na hilo, walitenganishwa na kufungwa katika magereza tofauti. Mabwana Kubai na Kaggia walionekana kuwa wenye misimamo mikali sana. Inaaminika kuwa waliamini kwamba Mzee Kenyatta alikuwa ameacha harakati za ukombozi na angekuwa kiongozi wa muda tu.

Mzee Kenyatta na Oneko walimchukulia Karumba kama ambaye hakuwa amesoma, lakini alijitolea sana kwenye harakati za ukombozi.

Oneko ndiye aliyewakutanisha Oginga Odinga na Mzee Kenyatta na kuwaingiza kwenye ulingo wa siasa. Alisisitiza kuhusu haja ya jamii ya Waluo kuungana na zile zingine kupigania uhuru.

Kufikia wakati wa kukamatwa kwake, Oneko alikuwa Katibu Mkuu wa chama cha Kanu, huku Mzee Kenyatta akiwa mwenyekiti.

Ni kutokana na wadhifa wake ambapo alipewa jukumu la kusafiri jijini Paris, Ufaransa pamoja na Mbiyu Koinange alikohutubu kuhusu siasa za kikoloni nchini Kenya na sera za kibaguzi za serikali hiyo.

Alirejea nchini bila Koinange, kwani aliamua kuendeleza masomo yake nchini Uingereza. Alimwarifu Mzee Kenyatta kuhusu mkutano huo.

Baadaye, alipewa kibali kuanza mikutano ya umma kote nchini kuwaeleza Wakenya kuhusu haja ya kubuni vyama vya kupigania uhuru na umuhimu wa kuwa huru.

Wakati Mzee Kenyatta alipoachiliwa kutoka kizuizini mnamo 1961, Oneko aliteuliwa kuwa msaidizi wa kibinafsi wa Mzee Kenyatta.

Baada ya uhuru, Oneko aliteuliwa katika Bunge la Wawakilishi, kuwakilisha mji wa Nakuru. Baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Habari na Utangazaji.

Kulingana na Oneko, mojawapo ya nyakati ngumu zaidi kwenye historia ya Kenya ilikuwa wakati uongozi wa chama cha Kanu uliwashawishi viongozi wa KADU kuondoka katika Upinzani.

Aliwakosoa vikali viongozi wa KADU kwa kushawishika virahisi kuacha chama chao kujiunga na Kanu, ili kuteuliwa kama mawaziri na Mzee Kenyatta.

Oneko alitumikia kifungo cha miaka 15 gerezani; kati ya 1952 na 1961, kwa imani yake kubwa aliyoonyesha kwa Mzee Kenyatta. Alitumikia kifungo chake cha pili kati ya 1969 na 1975. Katika kifungo chake cha pili, alikuwa pamoja na Odinga, aliyekuwa amehama kutoka Kanu na kubuni chama cha Kenya Peoples Union (KPU).

Odinga alichukua hatua hiyo baada ya kutofautiana na Mzee Kenyatta. Odinga aliachiliwa mnamo 1971, lakini Oneko alingoja hadi 1975.

Hata hivyo, maisha yake katika ulingo wa isiasa vile vile yalikuwa na nyakati nzuri, kwani alihudumu kama Katibu Mkuu wa KAU, mbunge wa Nakuru Mjini na Waziri wa Habari na Utangazaji.

Aliwahi kusema kuwa hizo ndizo nyakati alizofurahia zaidi.

Akikumbuka nyakati alizokuwa mfungwa, alisema: “Nikiwa kizuizini, tulikuwa na makubaliano kuwa baada ya uhuru, sera yetu ingekuwa kuupa umma nafasi ya kujikuza. Serikali ingewasaidia kujikuza kiuchumi. Lakini tulipoondoka kizuizini, Kenyatta alibadilika haraka. Ndipo mnamo 1966, ndimi nilikuwa wa mwisho kuhama Kanu na kujiunga na KPU. Nilimwambia kuwa wakati ulikuwa umefika kwetu kutengana.”

Wawili hao hawakuwa washirika tena, hadi baada ya miaka tisa. Serikali ya Mzee Kenyatta ilimfunga gerezani kwa miaka tisa katika magereza ya Kamiti, Naivasha na Manyani.

Baada ya kuachiliwa, alipelekwa katika Ikulu ya Nairobi, alikoshiriki mazungumzo na Mzee Kenyatta, Mwanasheria Makuu Charles Njonjo na Waziri wa Mipango ya Nchi Mbiyu Koinange.

Kabla ya kuondoka Ikulu, Oneko na familia yake walipewa usafiri wa bure kwenda nyumbani kwao.

Urafiki wao ukarejea tena. Oneko alisema kuwa Mzee Kenyatta aliagiza mawaziri watatu kuhakikisha kuwa walifika salama. Hiyo ndiyo ilikuwa mara ya mwisho kwa wawili hao kukutana. Mzee Kenyatta alifariki miaka mitatu baadaye.

Alimtaja Kenyatta kama “mpiganiaji uhuru wa kuheshimika.”

Hata hivyo, alisema kuwa hakutekeleza sera za serikali kama walivyokubaliana wakiwa kizuizini. Alisema kuwa uongozi wa Kenyatta “ulitekwa” na washirika wake, hasa kati ya 1973 na 1978.

Baadaye, alirejea katika ulingo wa siasa mnamo 1990. Aliwania ubunge katika eneobunge la Rarienda na kuibuka mshindi kwenye uchaguzi wa 1992.

Hata hivyo, alishindwa mnamo 1997, baada ya kukataa kujiunga na chama cha NDP, kilichoongozwa na Raila Odinga.

Alibaki katika chama cha Ford-Kenya hadi kifo chake mnamo Juni 9, 2007. Alifariki akiwa na miaka 87.

Alimwacha mjane, Bi Loise, na watoto 11. Mke wake wa kwanza alifariki mnamo 1992.

 

Kwa hisani ya Kenya Yearbook Editorial Board; kenyayearbook.co.ke

Habari zinazohusiana na hii