KINAYA: Ni njama tu ya kamati ya roho chafu kutaka kunyima Mwende kazi!
Na DOUGLAS MUTUA
JE, umeyasikia haya? Yepi tena? Kwamba ile kamati ya roho chafu isiyopenda kuona watu wakiendelea imekutana na kukubaliana kutompa kazi dada yetu.
Dada ya nani ilhali kila mtu ana kwao? Namzungumzia dada Mwende Mwinzi, mzaliwa wa Marekani mwenye asili ya Kitui, aliyeteuliwa balozi wa Kenya Korea Kusini.
Amekula mbuzi wa nani binti Mwende? Hata! Kawaida wajua hasidi hana sababu. Na hakuna kusanyiko lolote la mahasidi lililo kubwa kuliko kamati ya roho chafu.
Madai dhidi ya Mwende ni kwamba hawezi kuendelea kushikilia uraia pacha – wa Kenya na Amerika – kisha atarajie kupata kazi za serikali.
Kwa nini mtu anayejitolea kufanya kazi akatazwe ilhali duniani kumejaa wazembe wanaolaza damu mchana kutwa hali wanatarajia kulipwa?
Samahani, hii si kazi ya kawaida tunayozungumzia hapa. Si kuvuna kahawa wala majanichai wala kupika mahamri mtaani.
Si kazi ya kuwatolea mbwa ukoko chunguni wala ya kufagia barabara usiku kana kwamba mtu kaingia wazimu.
Hizo ni za makabwela, watoto wa mashambani tulioingia jijini juzi tu kujionea taa zinavyojiwakia usiku bila kutumia mafuta wala kuwashwa kwa kiberiti cha mtu!
Aliyoikamia ila ikampiga chenga Mwende ni kazi kubwa, yenye mshahara mnono na marupurupu ya kutamanisha, ya kumfanya mtu adondokwe na ute.
Oh! Kumbe ndiyo sababu dada mtu ameamua kuacha neema za kimarekani kuja kushindana na Wakenya wanaojiita wazalendo wa kweli eti? Sasa nimeelewa.
Nisichoelewa ni iwapo Mwende mwenyewe alidhani hakuna wazalendo wa kiwango cha juu kumzidi nchini Kenya, alitudharau, au alijiona bora kuliko wote.
Fikra kama hizo za kumdhania mtu mambo asiyosema mwenyewe ndizo ninazoita za kamati ya roho chafu, watu wanaoungulika zaidi ya kuungulika ukipata nao wakose.
Wako radhi tukose sote, tule vumbi na kwenda miayo, mradi wewe usipate. Ndio hao unaowasikia wakishangilia na kufurahia mkosi wa dada Mwende.
Mkosi? Mkosi gani? Mbali na kupokonywa nyama ya ubalozi ikiwa kinywani, alijaribisha siasa za Kitui katika uchaguzi wa 2017 akaambulia patupu!
Alianguka mwangwi ukasikika Marekani kwa Trump. Akwende huko! Kwani kwao Marekani hakuna vyeo vya kuwaniwa?
Si akajaribishe kumng’oa Trump madarakani katika uchaguzi wa mwaka ujao? Mbona asimuige Barry Obama, Mkenya stadi aliyeamua kuongoza Marekani badala ya kuja kushiriki siasa za chuki na ukabila kwenye taifa la baba yake?
Ile kamati ya roho chafu niliyokutajia itateta na kuuliza maswali mengi kama hayo huku ikiangua kicheko cha kishetani, nusura mbavu ziwateguke. Mahasidi!
Hebu tuelewane hapa: Binafsi sitaki Kenya iwakilishwe na mtu asiye na hakika ni Mkenya au ni raia wa nchi nyingine yoyote ile. Hata hivyo, nataka sheria iwafuatwe ilivyo.
Na sheria ya sasa haisemi chochote kuhusu balozi aliye na uraia pacha. Ni njama tu ya kamati ya roho chafu kutaka kumtungia msichana wa watu sheria ili imnyime kazi.
Nimesikia fununu kwamba watu wanaoishi ughaibuni wanajiandaa kwenda mahakamani kuuliza kwa nini wasiruhusiwe kuwania vyeo ilhali ni wazawa wa Kenya. Nitakuwa nao.
***
Vifo vimekuwa hali ya maisha nchini Kenya, watu wazima na watoto wakifa kama viroboto!
Habari za Kenya zinaweza kukupa msongo wa mawazo. Maisha hayana thamani; watu wanauana kwa kunyongana, kupondana vichwa na hata kuwadunga visu watoto wakiwa tumboni. Ukiwaza kuhusu hayo, darasa linaporomoka na kuwaua wanafunzi!