SHINA LA UHAI: Visa vya wanaume kujitoa uhai vyaongezeka ulimwenguni, kunani?
Na LEONARD ONYANGO
JE, kati ya wanawake na wanaume ni akina nani wana furaha zaidi ya wengine?
Hili ndilo swali watafiti wamekuwa wakijaribu kulielewa.
Utafiti uliofanywa na shirika la Gallup katika nchi 73 mnamo 2014, ulibaini kwamba wanawake ndio wenye furaha zaidi ikilinganishwa na wanaume.
Licha ya wanawake kuonekana kuwa wenye furaha, tafiti ambazo zimewahi kufanywa zinaonyesha kuwa idadi kubwa husumbuliwa na tatizo la mzongo wa mawazo ikilinganishwa na wanaume.
“Mzongo wa mawazo husababisha mtu kupoteza hamu ya kila kitu na kukasirika bila sababu. Mtu hushindwa kupata usingizi na hawezi kufikiria vyema. Mwathiriwa huwa na maumivu ya mgongo na kichwa,” anaelezea Dorcas Magai, mtafiti wa masuala ya kisaikolojia wa Taasisi ya Kutafiti Matibabu-KEMRI.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linataja mzongo wa mawazo kuwa kisababishi kikuu cha watu kujitoa uhai.
Lakini kinaya ni kwamba wanaume ndio wanaongoza kwa kujitoa uhai kote duniani, ikiwemo Kenya.
Kwa mfano, ripoti kuhusu Hali ya Uchumi nchini iliyotolewa na Shirika la Takwimu nchini (KNBS) mnamo 2018, inaonyesha kwamba kati ya watu 421 waliojinyonga mwaka 2017, wanaume walikuwa 330. Wanawake waliojiua walikuwa 91 pekee.
Kati ya watu 302 waliojiua 2016, wanaume walikuwa 224. Mnamo 2015, wanaume 177 walijiua ikilinganishwa na wanawake 44.
Lakini idadi ya watu wanaojiua huenda ikawa juu zaidi kwani visa vingi haviripotiwi.
Kulingana na Samuel Cheburet, mkuu wa usajili katika wizara ya Afya, visa ambapo waathiriwa hujiua kwa kugongesha magari yao huorodheshwa kama ajali za barabarani hivyo huwa vigumu kujua idadi halisi ya watu wanaojitoa uhai.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa kujitoa uhai ndicho kisababishi kikubwa cha vifo vya wanaume nchini Uingereza.
Nchini Australia, wanaume wanajitoa uhai mara tatu zaidi ikilinganishwa na wanawake.
Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa kila walipo wanaume 100,000, 15 kati yao wanawazia kujitoa uhai duniani.
Kenya imeorodheshwa katika nafasi ya 140 kote duniani kwa idadi ya watu ambao hujiua. Inakadiriwa kuwa kila palipo na watu 100,000, sita wanafikiria kujiua nchini Kenya.
Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa watu 800,000 hujitoa uhai kila mwaka kote duniani.
Data za shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa watoto 9,300 wa umri wa miaka 10 na 14 hujiua kila mwaka. Matineja 52,000 wa umri wa kati ya miaka 15 na 19 hujitoa uhai huku wengine 78,000 wa umri wa miaka 19 na 24 wakijiangamiza kila mwaka kote duniani.
Vifo vingi vya vijana wa kati ya umri wa miaka 15 na 29 hutokana na kujiua kote ulimwenguni, kwa mujibu wa WHO.
Kwa nini idadi kubwa ya wanaume hukimbilia kujiua ikilinganishwa na wanawake?
Utafiti uliofanywa katika mataifa ya bara Ulaya uligundua kuwa wanawake wanapofikiria kujiua, pia wanafikiria kuhusu madhara ya kufanya hivyo.
“Wanawake huanza kufiria watoto wao watabaki vipi, jamii itachukuliaje watoto wake na hivyo kuna uwezekano wa kuachana na azma yake ya kutaka kujitoa uhai,” ukasema utafiti huo.
“Lakini wanaume wanapoamua kujitoa uhai, ni vigumu kubadili nia yao. Kadhalika wengi wao hutumia mbinu hatari zaidi kama vile kujifyatulia risasi, kujinyonga na kadhalika, ikilinganishwa na wanawake ambao hutumia mbinu zisizo za fujo kama vile kumeza tembe au kunywa kemikali za kuua wadudu,” ikaongezea ripoti hiyo.
Matumizi ya mihadarati na pombe pia zinachangia katika watu kujitoa uhai.
Matokeo ya utafiti uliofanywa na shirika la Trust for America’s Health and Well Being, yalionyesha kuwa mihadarati inachangia pakubwa kwa wanaume kujiua haswa vijana wa kati ya umri wa miaka 18 na 34.
Kulingana na utafiti huo, matumizi ya mihadarati na pombe huongeza mzongo wa mawazo ambao husababisha mwathiriwa kuanza kuwaza kujitoa uhai.
Matumizi ya mihadarati na pombe ni miongoni mwa sababu kuu ambazo zimelaumiwa kutokana na ongezeko la watu kujitoa uhai katika eneo la Mlima Kenya, Nyanza na Pwani.
Wanawake hupendelea zaidi kuzungumzia masaibu yanayowakumba ikilinganishwa na wanaume ambao huyanyamaza na kuweka fundo moyoni.
“Kulingana na tamaduni za jamii nyingi, wanaume huchukuliwa kuwa wajasiri na wakakamavu na kuzungumzia matatizo yanayowazonga huwafanya kuonekana wanyonge,” anasema Bi Magai.
“Mara nyingi hili huanzia utotoni ambapo wavulana huambiwa kwamba wanaume hawafai kulia, hivyo watoto hukua wakijua kwamba hawaruhusiwi kuonyesha hisia zao,” anaongezea.
Wataalamu wa masuala ya kisaikolojia pia wanasema kuwa akina mama hupendelea kuzungumza mambo mengi na binti zao na kuwategea mgongo wavulana.
Aidha wanaume huona haya kukiri kwamba wanapitia changamoto na wengi wao hufichua ikiwa tayari wameshakata tamaa maishani.
Wataalamu wanasema kuwa huwa ni vigumu kwa wanaume kutafuta huduma za matibabu wanapohisi kuwa na mzongo wa mawazo.
Utafiti uliochapishwa katika jarida la British Medical Journal ulibaini kwamba ni asilimia ndogo mno ya wanaume nchini Uingereza wanaotafuta huduma za wataalamu wa ushauri nasaha ikilinganishwa na wanawake.
“Wanawake na wanaume hupitia changamoto sawa maishani. Lakini wanawake hupendelea zaidi kutafuta huduma za wataalamu wa ushauri nasaha ikilinganishwa na wanaume,” ikasema ripoti hiyo.
Mtaalamu wa afya ya ubongo, Dkt Frank Njenga anasema kuwa watu ambao wamewahi kujaribu kujiua, wako katika hatari kubwa ya kujitoa uhai.
Dalili za mwanamume mwenye msongo wa mawazo:
Kuonekana mwenye huzuni
Kukasirika haraka
Kupoteza hamu ya chakula
Kukosa hamu ya kufanya kazi
Kushindwa kufanya maamuzi
Kuhisi asiyekuwa na thamani
Kufikiria mambo mabaya kama vile kujiua
Tabia zisizo za kawaida kama vile kuendesha gari kiholela, kutaka kupigana bila sababu, ulevi, kujikita kwenye michezo ya kamari
Kukosa hamu ya tendo la ndoa
Upweke
Maumivu ya mgongo, kichwa na matatizo mengineyo ya kiafya
Kiini
Urithi kutoka kwa wazazi/kiukoo
Hali ngumu ya maisha
Kuhangaishwa kazini
Matatizo katika ndoa/mapenzi
Matatizo ya afya
Ukosefu wa fedha
Kustaafu bila kujijenga kimaisha
Kufiwa
Kukosa uwezo wa kutekeleza tendo la ndoa kitandani (ubwege)
Masaibu ya utotoni
Matumizi ya mihadarati/pombe
Kuepuka mawazo ya kujiua
Zungumza na mtu unayemwamini
Wataalamu wanashauri kuwa ili kuepuka kuwa na hisia za kutaka kujiua, mwathiriwa anafaa kutafuta mtu anayemwamini na kumwelezea changamoto anazopita.
Dkt Njenga anashauri kuwa ni vyema kukutana na mtu ana kwa ana na kumwelezea changamoto zilizopo badala ya kupiga simu, kutuma arafa au kumwaga hisia kwenye mitandao ya kijamii.
“Kitendo cha kuzungumza na mtu ana kwa ana husaidia pakubwa katika kupunguza msongo wa mawazo,” anasema.
Fanya mazoezi
Mazoezi pia ni silaha tosha ya kukabiliana na msongo wa mawazo. Wataalamu wanasema kuwa kufanya mazoezi na watu wengine hupunguza mawazo ambayo husukuma watu kujitoa uhai.
Fanya hisani
Tafiti zinaonyesha kuwa kuwasaidia watu wengine pia kunasaidia mtu kuhisi vyema. Unapowasaidia watu na hata kusikiza masaibu wanayopitia, hukufanya kuelewa kwamba changamoto zinazokukumba si kitu.
Tangamana na watu
“Ikiwa wewe ni mpenzi wa kutazama filamu, kandanda, na kadhalika, alika rafiki mtazame naye. Hapo mtapata fursa ya kujadili namna ya kutatua changamoto mbalimbali zinazowakumba,” wanasema wataalamu.
Kula ipasavyo
Watafiti wanasema kuwa kula kwa muda mfupi chini ya saa nane kwa siku ni hatari kwa afya na kunaweza kusababisha mzongo wa mawazo.
Ota jua
Wataalamu wa afya ya akili pia wanashauri kuwa kutoka nje na kuota jua asubuhi kunapunguza mzongo wa mawazo. Mwangaza wa jua husisimua homoni za serotonin ambazo hufanya mtu kuonekana mwenye furaha.
Punguza sukari
Chakula kisichokuwa na sukari nyingi pia husaidia kupunguza mzongo wa mawazo.
Punguza vyakula vyenye kafeni
Punguza au achana na vyakula ambavyo hubadili hisia kama vile kahawa, mvinyo na vyakula vilivyo na kemikali nyingi.
Tumia mafuta ya Omega 3
Mafuta ya samaki, maarufu Omega 3 pia yanasadikiwa kumfanya mtu kuhisi mwenye furaha.
Madini ya magnesia
Vyakula vilivyo na madini ya magnesia kama vile ndizi na mboga aina ya spinachi hupunguza hali ya wasiwasi akilini hivyo kumfanya mtu kuwa mtulivu.