• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
Bi Galgalo aidhinishwa NLC kipindi cha lala salama

Bi Galgalo aidhinishwa NLC kipindi cha lala salama

Na CHARLES WASONGA

HATIMAYE wabunge wameidhinisha uteuzi wa aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Isiolo Bi Tiya Galgalo kuwa mwanachama wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) kwa kujumuisha jina lake kwenye ripoti ya kamati ya ardhi dakika za mwisho.

Sasa jina la Bi Galgalo pamoja na watu wengine wanane waliopendekezwa na Rais kushikilia nyadhifa za mwenyekiti, na makamishna wa tume hiyo yatawasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta ili awateue rasmi.

Gershom Otachi atashikilia wadhifa wa mwenyekiti nao aliyekuwa Mbunge wa Nyeri Mjini Esther Murugi Mathenge, Bi Getrude Nguku, Mbw Reginald Okumui, Elister Mutungi, Hubbie Husseni Ali, aliyekuwa Waziri wa Leba Samuel Kazungu Kambi na aliyekuwa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Egerton Profesa James Tuitoek wakiwa makamishna.

Awali, ripoti ya kamati hiyo iliyowasilishwa na mwenyekiti wa kamati hiyo Rachael Nyamai, ilikosa kuidhinisha jina lake kwa misingi kwamba hakuwa ametimiza masharti ya ulipaji wa ushuru kamati hiyo ilipompiga msasa wiki iliyopita.

“Kamati hii ilimkataa Bi Galgalo kwa sababu chetu cha ushuru kutoka Mamlaka ya Ushuru Nchini (KRA) ambayo aliwasilisha mbele yetu tulipokuwa tukimpiga msasa ilikuwa feki,” akasema Dkt Nyamai.

Kukatiliwa kwa cheti hicho kulimaanisha kuwa Bi Galgalo hangeruhusiwa kushikilia wadhifa wa umma kulingana na hitaji la Sura ya Sita ya Katiba kuhusu maadili na maongozi mema kwa watumishi wa umma.

Lakini Jumanne, Dkt Nyamai aliliambia bunge kuwa kamati yake ilipokea barua nyingi kutoka kwa KRA ikisema kuwa Bi Galgalo sasa ametimiza masharti yote ya ulipaji ushuru.

Ni kwa misingi ya barua hiyo ambapo Mbunge wa Isiolo Kaskazini Hassan Oda Hulufo aliwasilisha hoja maalum ya kujumuisha jina la Galgalo kwenye orodha ya watu nane walioidhinishwa na Kamati hiyo ya Dkt Nyamai.

Hoja hiyo ilipita kwa kura 114 dhidi ya 70 za wabunge waliopinga hatua hiyo.

You can share this post!

Apinga pendekezo la kuondoa neno ‘harambee’...

Ubingwa wa mapema waisubiri Kinyago

adminleo