Michezo

Afueni Arsenal, Manchester united wakila sare EPL

October 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

ARSENAL wamerejea kwenye kundi la timu nne-bora kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kutoka sare 1-1 na Manchester United katika pambano kali lililowakutanisha Jumatatu usiku.

Wakiwa nyumbani ugani Old Trafford, Manchester United walitangulia kufunga bao kupitia kwa kiungo Scott McTominay katika dakika ya 45.

Lakini Pierre-Emerick Aubameyang aliwarejesha Arsenal mchezoni kwa kupachika wavuni bao la kusawazisha kunako dakika ya 58.

Bada ya kucheza mechi saba, Man-United ipo katika nafasi ya 10 na alama tisa, haya yakiwa ni matokeo mabaya zaidi katika kipindi cha miaka 30 ya historia yao kwa kushindwa angalau kufikisha alama 10. Mara ya mwisho Man-United kuwa na matokeo kama haya mnamo 1989-90, walimaliza kampeni za ligi katika nafasi ya 13. Kwa mara ya kwanza kutoka mwaka wa 2000, Arsenal ilinusurika kupokea kichapo wakiwa ugani Old Trafford katika mechi mbili mfululizo za EPL. Pia Arsenal ilipiga mashuti mengi zaidi yaliyolenga shabaha (5) dhidi ya Man-United (4) katika dimba hilo kutokea mwaka wa 2009.

Arsenal wana alama 12, Man-United tisa, jumla yao ni alama 21, sawa na pointi za Liverpool ambao wapo kileleni.

Huu ulikuwa ni mchezo wa 28 wa ligi kwa Solskjaer kama kocha wa Man-United, na kwa ujumla wake amekusanya alama 49, ikiwa ni alama mbili pungufu ya zile alizoshinda Jose Mourinho katika mechi zake 28 za mwisho.

Solskjaer, amesema baada ya mchezo huo kuwa wana somo kubwa la kujifunza kutokana na matokeo hayo: “Mara ngapi tumekuwa tukiongoza 1-0 na tumeshindwa kufunga goli la pili? Tuna bonde refu la mambo ya kujifunza, na tutaendelea kufanya kazi kwa bidii, kwa uzoefu zaidi tutafanya maamuzi sahihi.”

“Hatukujituma ipasavyo mwanzoni mwa kipindi cha pili. Arsenal walijitoa kwa nguvu na kupata bao,” amesema Solskjaer na kuongeza, “Nilidhani tungeweza kupachika goli la pili mwishoni mwa mchezo, tulishambulia sana. Nimeshawahi kuwa katika hali kama hiyo nikiwa mchezaji, ambapo baada ya mchezo unahisi kuwa ungeweza kufanya vyema zaidi, lakini tutaendelea kujifunza.”

Kwa upande wake kocha wa Arsenal Unai Emery amesema bado anataka matokeo bora zaidi kutoka kwa wachezaji wake: “Tuliingia uwanjani kushindana na tungeweza kufanya vyema zaidi. Tunaweza kumiliki mchezo zaidi na kutengeneza nafasi za kushinda. Tuna wachezaji wadogo ambao wanaweza kujiamini zaidi.”