AKILIMALI: Alijitengenezea jina kwa uchoraji wake stadi wa maduka ya M-Pesa
Na STEPHEN ODANGA
KWA kawaida mchoraji huchukuliwa tu kama mtu wa kazi za mikono lakini ukweli ni kwamba pia yeye huwa ni msanii.
Mchoraji ni msanii wa sanaa ya uchoraji kwa sababu anaweza kukuangalia tu kwa sekunde chache na kuenda kukuchora vile vile ulivyo bila kukosea mahali.
Kijana anayefahamika kwa jina Wadegu Wilkey Owilla ama jina kwa lingine ‘’Wilsky Lorgan’’ ni mchoraji stadi anayesifika kwa kituo cha biashara cha Nyangweso, eneobunge la North Gem, Kaunti ya Siaya.
Msanii Wilsky Lorgan anasema kwamba yeye hakufunzwa na mtu yeyote, pia hakuenda katika chuo chochote cha mafunzo ya uchoraji bali ni kipaji cha kifamilia.Anafichua kwamba babu yake aliyemzaa mama alikuwa akifanya kazi ya kuchora na ndio amerithi talanta hii kutoka kwake.
Anasimulia kwamba wakati akiwa shuleni alipenda sana kuchora picha kwa daftari lake, kwa mfano alichora watu, magari, ndege na wanyama wa kila aina. Hii ilikuwa ni njia moja ya kujinoa na hata alipoingia kwa shule ya upili, walimu wa shule hiyo ya upili ya Kanyamedha, kaunti ya Kusumu waligundua kipawa chake.
Walimu waligundua kipawa alipofika kwa kidato cha nne mwaka wa 2016 na kumtia moyo zaidi na zaidi.Walimu walimshauri kwamba talanta hiyo ya uchoraji inaweza kuwa kitega uchumi maishani akishakamilisha masomo.
Mwaka wa 2018, mwaka mmoja baada ya kumaliza masomo ya shule ya upili, alifanikiwa kupata kazi ya kuchora katika duka moja la M-pesa jijini Kisumu ambako walikuwa wakiishi.
Alichora vizuri zaidi duka hilo la M-pesa na kisha kuweka nambari zake ambazo wateja wengi walimpigia simu walipofurahia kazi hiyo aliyofanya.
Msanii Wilsky Lorgan anasema kwamba duka moja la M-pesa alikuwa akichora kwa Sh1, 500 na aliweza kuchora maduka zaidi ya kumi na kupata pesa nyingi.
Baada ya hapo alionelea ni heri aende kwao mashambani kufungua karakana yake kwa sababu jijini Kisumu palikuwa na ushindani mkubwa,wachoraji walikuwa wengi zaidi. Alitumia pesa ambazo alipata kwa kazi za kuchora maduka ya M- pesa kama mtaji wa kufungua karakana kwa soko la Nyangweso, kaunti hii ya Siaya ambako yuko sasa.
Katika karakana yake anafanya shughuli nyingi za uchoraji kama vile kupaka rangi maduka, kuchora mabango na mashati- tao, kufanya dye, kuunda beji za shule na Art gallery miongoni mwa shughuli zingine.
Msanii Wilsky Lorgan anafichua kwamba kwa siku moja huunda kati ya Sh1,000 na Sh5,000 jambo ambalo limemtia moyo zaidi kwa hii kazi yake.
Anaongeza kusema kwamba yeye hawezi kuenda kuomba kazi mahali kwengine kwa sababu talanta yake yamtosheleza mahitaji yote.