Kimataifa

Kanisa Katoliki lina uhaba wa mapadri – Maaskofu

October 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

ITAITUBA, Brazil

Na MASHIRIKA

MAASKOFU wa Kanisa Katoliki katika mataifa ya Kusini mwa Amerika, wameonya kuwa kuna uhaba wa mapadri unaofanya kanisa kufifia Brazil na Peru huku wakipanga mkutano mkubwa eneo hilo kujadili suala hilo

Wilmar Santin, mmoja wa maaskofu wanaopanga kuhudhuria mkutano huo wa Oktoba 6 hadi 27 anasema kanisa linapoteza washirika kwa madhehebu ya Kievanjelisti na linapaswa kubadilisha mbinu.

“Ni yapi mapya tunayoweza kuwapa washiriki wetu ili waweze kubaki hapa na kuacha kuhamia kwa majirani,” aliuliza Santin ambaye anasimamia eneo linalotoshana na Ujerumani kwa ukubwa.

“Hii ni kwa sababu hatuwapi kondoo wetu malisho au hatulindi malisho inavyopaswa. Tumeshindwa kufanya hivyo,” alisema.

Aliambia wanahabari wa AFP kwamba kusajili watu wengi kutoka eneo hilo kuwa mapadri kunaweza kusaidia kuimarisha hali ya kanisa jambo ambalo anasema linawezekana walikubali mafunzo ya kanisa kwanza.

Ni wanaume wachache wazaliwa asilia wa Brazil ambao wametawaza mapadri.

Mbinu nyingine itakayojadiliwa katika mkutano wa maaskofu ni kuruhusu wanaume waliooa kutawazwa mapadri katika maeneo ya mbali na yaliyo nyuma kimaendeleo kama vile eneo la Amazon.

Papa Francis amenukuliwa mara kwa mara akisema kwamba hakuna kanuni ya kimafunzo inayowazuia wanaume waliooa na kufikisha umri fulani kuwa mapadri.

Abadili nia

Hata hivyo, mapema mwaka 2019 alionekana kubadilisha nia kwa kusema kwamba utauawa ni “zawadi kwa kanisa.”

Alikiri kuwa msimamo huu unaweza kulegezwa kwa maeneo ya mbali kama visiwa vya Pacific au Amazon ambako kuna haja ya kufanya hivyo lakini akaongeza kuwa sio yeye anayefaa kufanya uamuzi huo.

Santin anasema mapadri 21 na wasaidizi watatu huwa wanahudumia dayosisi ya Itaituba yenye ukubwa wa kilomita 175,365 mraba na ina miji sita mikubwa.

“Hii ni idadi ndogo kwa mahitaji yaliyopo,” alisema Santin akiongea na AFP katika makao yake Itaituba, mji ulio jimbo la Para.

Ingawa Brazil ingali nchi iliyo na idadi kubwa ya Wakatoliki ulimwengui, waumini wamepungua huku makanisa ya kievanjelisti na kiprotestanti yakikua.

Kulingana na sensa ya mwaka wa 2010 asilimia 64 ya raia walijitambulisha kama Wakristo tofauti na asilimia 74 kwenye sensa ya 2000.

Askofu David Martinez raia wa Uhispania anayehudumu Puerto Maldonado, Peru anasema kwa kuwa idadi ya mapadri kutoka Ulaya wanaoenda kufanya kazi ya umishonari eneo hilo imepungua, kuna haja ya kusajili wazawa asilia.

“Hatutaki kuwa kanisa la kujenga makanisa mengine, tunataka kuwa kanisa la kudumu,” Martinez ambaye ni katibu wa muungano wa maaskofu wa eneo la Amazon aliambia wanahabari akiwa Peru.

“Kanisa linataka wazaliwa asilia wa eneo la Amazon kuliongoza, kuhisi kanisa kuwa lao na sio la wageni,” alisema.