Mkewe Cohen kujua hatima ya ombi la dhamana Oktoba 11
Na RICHARD MUNGUTI
MKEWE aliyekuwa mfanyabiashara tajiri Tob Cohen, Sarah Wairimu Kamotho atakaa gerezani kwa wiki moja kabla ya kujua iwapo ataachiliwa kwa dhamana au la.
Ijumaa mahakama iliahirisha uamuzi wa ombi lake la dhamana hadi Ijumaa wiki ijayo. Sarah aliyekanusha shtaka la kumuua mumewe mnamo Julai 19/20, 2019 aliambia mahakama kwamba upande wa mashtaka haujampa mshukiwa huyo nakala za mashahidi.
“Kufikia sasa ni siku 38 lakini hakuna hata chembe ya ushahidi tuliyopewa na upande wa mashtaka ya kumhusisha mshtakiwa na mauaji ya mumewe,” Bw Murgor alimweleza Jaji Mutuku aliyeamuru ombi hilo lisikizwe mara moja.
Bw Murgor alisema kwa kuwa upande wa mashtaka haujamkabidhi ushahidi, basi itachukuliwa kuwa hakuna sababu zitakazotegemewa na upande wa mashtaka kukataa mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.
Wakili huyo aliomba mahakama imwachilie mshtakiwa akaendeleze biashara yake iliyofungwa tangu alipotiwa nguvuni.
“Biashara ya Sarah inakabiliwa na tishio la kufungwa kwa kuwa wafanyakazi wake walitimuliwa,” alisema Bw Murgor.
Lakini Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) alipinga ombi hilo akisema mshtakiwa hapaswi kuachiliwa kwa dhamana kwa kuwa atawavuruga mashahidi na kuwatisha wasifike kortini kutoa ushahidi.
Kiongozi wa Mashtaka, Bi Wangui Gichuhi alisema tayari ndugu na dada wa marehemu Bernard na Gabrielle wameelezea hofu yao iwapo Sarah ataachiliwa.
“Ikiwa mshtakiwa ameweza kuishi akijua maiti ya mumewe iko ndani ya tanki kwa siku 60 hadi ilipopatikana, inamaanisha ni mtu hatari na kile kinachofaa ni anyimwe dhamana hadi kesi iamuliwe,” alisema wakili Cliff Ombeta anayewakilisha familia ya mhanga.