• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Wizara yaagiza kufungwa kwa shule 22 Kisumu

Wizara yaagiza kufungwa kwa shule 22 Kisumu

Na CHARLES WASONGA

WIZARA ya Elimu imeamuru kufungwa kwa shule 22 katika Kaunti ya Kisumu kwa kufeli kuzingatia kanuni za usalama kulingana na Sheria ya Elimu.

Mkurugenzi wa Elimu katika kaunti hiyo Isaac Atebe alisema Ijumaa kuwa shule moja katika kaunti ndogo ya Nyando tayari imefungwa akiongeza kuwa mchakato wa kufunga zingine 21 unaendelea.

Ukaguzi unaoendelea umebainisha kuwa majengo katika shule 22 katika kaunti hiyo hayako salama kwa matumizi ya wanafunzi kwani hayakujengwa kulingana na kanuni za ujenzi.

“Katika eneo la Ahero, kaunti ndogo ya Nyando, shule moja ya binafsi ilipatikana na majengo yenye nyufa ndiposa tukaamuru ifungwe,” Bw Atebe akasema.

Aliongeza kuwa shule kadhaa zimekuwa ziendesha shughuli zao bila kusajiliwa na Wizara ya Elimu.

“Ilani ya kufungwa kwa shule husika inalenga kuwaruhusu wanafunzi kusaka nafasi katika shule za umma zilizoko karibu kulingana na mapenzi ya wazazi wao,” Bw Atebe akaeleza.

Afisa huyo alisema kikosi cha maafisa kutoka afisi yake kimekuwa kikizuru shule za umma na za binafsi kukagua ikiwa zimezingatia kanuni hitajika kama ilivyotangazwa na Waziri wa Elimu Profesa George Magoha.

Hii ni kufuatia kuporomoka kwa darasa katika shule ya Precious Talent Academy, Dagoretti, Nairobi ambapo wanafunzi wanane walifariki na wengine 54 wakajeruhiwa.

You can share this post!

Polisi wachunguza kifo tata cha dadake mbunge wa Githunguri

TAHARIRI: Sekta ya michezo inahitaji suluhu

adminleo