Makala

MWANAMUME KAMILI: Ni ugumegume kufikiria haja ya mke ni chumbani tu!

October 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na DKT CHARLES OBENE

NILIPOKUWA kwenye matatu moja mtaani, nilidakia kwa huzuni mazungumzo ya wanaume walioketi nyuma yangu.

Hawakuwa watoto watu wale ila mazungumzo yao hayakuwa mbali mno ya semi ya watoto wa chekechea. Kwani? Walitamka kwa uzito na ukakamavu kwamba “wanawake hawana haja na jambo lingine ila kutimiziwa haja za chumbani tu!”

Sijui kama hilo ndilo alilotazamia mamangu kwa miaka yote hiyo aliyovumilia dhiki za kuolewa na mngwana babangu! Sitaki kuwa mtovu wa adabu kudadisi mambo ya wazee hao lakini sitachelea kusema mengi juu ya akili duni zilizokita fuvuni mwa baadhi ya wanaume wa leo.

Sawia na walivyosema wangwana wazee wa jadi kwamba mkono mtupu haulambwi, ndivyo ilivyo ada ya ngoma yenye mrindimo kupigwa. Ole nyinyi wanaume wa leo mnaodhani kwamba wanawake – hasa wa karne hii – wanaweza kujisitiri kwa ukavu wa vitanga na viganja vyenu maadamu haja za chumbani zimetimizwa. Akili sampuli hiyo sizo za kiume!

Ninaangazia wazo hili la “kutimiziwa haja za chumbani” kwa maana wengi wa malofa wa leo wamepotoka kwalo. Watu wazima hawa wameshikilia kikiki kwamba mke hana matarajio mengine kimaisha ila hilo la “kutimiziwa haja za chumbani tu!” Sina hakika wala sina haja kujua zaidi ya hali ilivyo.

Isitoshe, sina haja kudunisha hekima ya wanaume wa leo ila sikubali kamwe hadaa na ngebe za mabahili na wazembe wasiotaka kufika viwandani ama mashambani kuzumbua riziki kwa masilahi ya familia.

Mwanamke yupi akijua vyema hadhi yake anaweza kukubali daima kula maponeo, kuvalia magwanda ama kulalia mikeka kwa kuridhia haja ya mume? Nionyesheni mmoja kati ya lulu hawa ambaye kwa akili zake timamu anaweza kula na kulalia mahaba; akaamkia na kushinda kwayo! Jamani tuziacheni hizi dhana za kitoto kupotoka kwa vijimambo visivyokuza wala kustawisha familia na jamii.

Tuziachie mbali hizi hekaya za walevi wa gongo na majani ya miti asili. Tusimameni wima kufanya analohitajika mume kulifanya ili kuipa familia sura na hadhi. Mume si mume pasipo kufanya jitihada kukidhia mahitaji ya familia. Kazi ya mwanamume ni kuilinda, kuitetea na kuifanikisha familia yake. Ulinzi, utetezi na mafanikio hayataafikiwa pasipo mume kukuza mawazo chanya na kufanya bidii kwa lolote lile. Iwe kazi iwe bazi, sharti kuliwajibikia. Hivyo ndivyo afanyavyo mwanamume kamili

Sina haja kuwahukumu wala sababu yoyote kuwatetea wanawake wa leo. Lakini wakati mwingine tunawafanya mabozi wasiojua mengi ya karne hii. Udunishani wa haki na masilahi ya wanawake ni mbinu tu ya malofa na wazembe kukwepa kufanya kazi za tija kufurahisha wanawake na watoto wao. Lau wanaume wa leo wangaliwajibikia kukuza maadili, nani asingalikuwa na mke mwema, mtiifu tena aliyeradhi “kutimiziwa haja za chumbani?”

Sijasahau kile kisa cha mwanamume aliyeshikwa katika hospitali ya Kitaifa humu nchini akifanya kila jambo kumwokoa mkewe na mwanawe waliokuwa wamezuiliwa kwa kushindwa kulipa ada ya matibabu. Siko hapa kuunga mkono wizi ama hila kama hizo. Lakini yule alikuwa mume kwa ari yake! Ndio maana mahakama haikuwa na budi ila kumwachilia huru! Alifanya kosa ila kusudi lake lilikuwa jema. Hayo ndio mawazo ya mwanamume kamili.

Kuwa mfano mwema

Mwanamume kamili hana budi kumpa mke mfano mwema! Mawaidha na nasaha zitakazomfanya mtu wa hadhi mbele ya watu, tena mke wa thamani! Ithibati ya upendo ni kudumisha nidhamu na heshima kwanza kabla kutanguliza mbele jazba.

Mume mwenye kumpangia mkewe ngoma za chumbani kana kwamba ni hawara bila shaka ni gumegume! Jamani, mtoto wa kike hana haja kugeuzwa jamvi kwa mapigo na mapapo! Kwanza mfanye mke mbele ya wake wengine kabla hizo jazba za kila uchao!

Sifa za mnyama ni kufanya mambo bila tafakari. Sisi binadamu, watu wenye akili timamu mbona tabia za kinyama? Jamani tatizo nini kufikia hatua ya kugeuka hayawani na akili tunazo?

Kwa mtindo huu wa wanaume kuzembea na kutowajibikia familia na jamii zao tutasalia wanaume wanaoombaomba kila kitu tena kutoka kila mtu! Tusijeshangaa kuona wenye mali na hadhi wakija mchana wa jua na kutufunza adhabu akina sisi tunaodhani kwamba matarajio ya mke ni “kutimiziwa haja za chumbani tu!” Hamna budi kubadili akili na fikra zenu duni!

 

[email protected]