• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
TAHARIRI: Tatizo si sheria kukabili pombe bali uzingatiaji

TAHARIRI: Tatizo si sheria kukabili pombe bali uzingatiaji

Na MHARIRI

WITO wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Pombe na Mihadarati (Nacada) kuhusu hitaji la mabadiliko ya sheria za pombe, huenda lisifanikiwe kuleta mabadiliko mengi hata likitelekezwa.

Kwa miaka mingi tunapopatwa na tatizo la kiusimamizi katika nchi hii, huwa viongozi na maafisa serikalini wanaharakisha kujaribu kubuni sera na sheria mpya.

Jambo hili huwa linaonekana katika sekta tofauti wakati wowote kukiwa na misukosuko.

Kile ambacho huenda wengi hawatambui ni kwamba, licha ya mabadiliko ya kisheria au sera kufanywa mara kwa mara, huwa ni nadra kuona hali nafuu kwa kile kinacholengwa kurekebishwa.

Kwa msingi huu, ni wazi kwamba tatizo linalotukumba huwa halihusu sera na sheria bali watu waliotwikwa jukumu la kutekeleza sheria na sera hizo.

Tukichukua mfano wa sekta ya utengenezaji na uuzaji wa pombe, kuna sheria tele zilizo thabiti katika serikali kuu na vile vile katika serikali za kaunti.

Si siri kwamba hii ni mojawapo ya sekta ambazo baadhi ya maafisa serikalini hutumia kujitajirisha kupitia kwa ulaji rushwa.

Kuanzia kwa utoaji leseni za biashara ya pombe hadi utengenezaji na uuzaji wa pombe haramu, hutakosa maafisa wa serikali wakihusika katika ukwepaji wa sheria zilizonuiwa kudhibiti sekta hii.

Sheria tunazo kuhusu mahali ambapo biashara ya pombe inafaa kufanywa na vile biashara hiyo inastahili kuendeshwa, lakini unapotembea katika miji karibu yote ya nchi hii, hizo sheria zinapuuzwa mchana peupe!

Vijijini nako, sheria zipo za kukabiliana na utengenezaji na uuzaji wa pombe haramu, lakini hali si hali kwani kuna machifu na polisi ambao husemekana kulinda wale wanaofanya biashara hiyo haramu inayosababisha madhara kwa raia kila kukicha.

Hivyo basi, badala ya Nacada kuanza kushinikiza mabadiliko ya kisheria, ni bora shirika hilo lianze kwa kufanya utathmini kuhusu vikosi vilivyopewa jukumu la kutekeleza sheria zilizopo.

Bila hili, tutashinda tukibadilisha sheria kila mara ila hatutaona mabadiliko yoyote ya kufana. Itakuwa sawa na msemo maarufu wa kubadilisha misitu ilhali tumbili ni wale wale!

You can share this post!

Ruto akaidi agizo la maaskofu Wakatoliki

DIMBA: Saka; kinda wa Arsenal

adminleo