• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 11:13 AM
DIMBA: Saka; kinda wa Arsenal

DIMBA: Saka; kinda wa Arsenal

Na CHRIS ADUNGO

JAMBO ambalo wachanganuzi wengi wa soka nchini Uingereza wanakiri kwamba litafanikisha kampeni za Arsenal msimu huu, ni jinsi walivyojishughulisha katika soko la uhamisho wa wachezaji katika kipindi cha mihula miwili iliyopita.

Katika miaka ya hivi karibuni, Arsenal wamekuwa wakipungukiwa na idadi nzuri ya wachezaji wa kujitolea, wenye uwezo wa kukipigania kikosi kwa jino na ukucha kwa nia ya kuwavunia ushindi katika takriban mechi zote.

Safu ya kati ya Arsenal imekuwa ikikosa kabisa huduma za wachezaji wenye nguvu na pumzi zisizokwisha kwa urahisi kila wanapowajibishwa uwanjani.

Tangu kubanduka kwa nahodha Patrick Vieira, aliyekuwa kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, alishindwa kabisa kuziba pengo la kiungo huyo mzawa wa Ufaransa aliyeagana na kikosi hicho mnamo 2005. Vieira kwa sasa ni kocha wa klabu ya Nice nchini Ufaransa.

Tangu ujio wa mkufunzi Unai Emery, mambo yameanza kubadilika uwanjani Emirates kwa kiwango fulani. Sura mpya za wachezaji wachanga wenye kiu ya kujituma vilivyo zimeanza kujitokeza.

Isitoshe, urafiki na ushirikiano mkubwa kati ya Alexandre Lacazette na Pierre-Emerick Aubameyang katika safu ya mbele ya Arsenal ni jambo linatarajiwa kuwakosesha wapinzani usingizi kwa muda mrefu ujao.

Hatua ya Emery kuwasajili wachezaji Matteo Guendouzi na Lucas Torreira imekuwa kiini cha kuboreka zaidi kwa ngome ya Arsenal ambayo itasalia kubebwa na chipukizi tele wanaojivunia utajiri mkubwa wa vipaji.

Bukayo Saka, 18, ni mvamizi chipukizi mzawa wa Uingereza ambaye kwa sasa huvalia jezi za Arsenal katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Kwa pamoja na Eddie Nketiah, Reiss Nelson, Gabriel Martinelli, Kieran Tierney na Joe Willock, Saka ni miongoni mwa wachezaji wachanga wanaobeba mustakabali wa Arsenal migongoni mwao.

Akiwa mzaliwa wa jiji la London, Saka alianza kutandaza soka kitaaluma katika akademia ya Hale End inayomilikiwa na Arsenal nchini Uingereza.

Alipohitimu umri wa miaka 17, alipokezwa mkataba wa kudumu na Arsenal kisha kukwezwa kuwa sehemu ya kikosi cha wachezaji wasiozidi umri wa miaka 23 (Under-23) uwanjani Emirates.

Mnamo Novemba 29, 2018, Saka aliwajibishwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha watu wazima kambini mwa Arsenal. Mchuano huo ni kibarua kilichowakutanisha na Vorskla Poltava ya Ukraine katika kivumbi cha kuwania ufalme wa taji la Europa League.

Alitokea benchi na kuingia uwanjani katika dakika ya 68 kujaza nafasi ya kiungo mzawa wa Wales, Aaron Ramsey ambaye kwa sasa ni mali rasmi ya Juventus nchini Italia.

Mnamo Disemba 13, 2018, Saka aliunga kikosi cha kwanza cha Arsenal na kuwajibishwa kwa dakika zote 90 katika mchuano wa Europa League dhidi ya FK Qarabag inayoshiriki Ligi Kuu ya soka nchini Azerbaijan.

Mechi yake ya kwanza ya EPL ndani ya jezi za Arsenal ni kipute kilichowakutanisha na Fulham mnamo Januari 1, 2019.

Katika mchuano huo uliowashuhudia wakisajili ushindi wa 4-1 mbele ya mashabiki wao wa nyumbani uwanjani Emirates, Saka alitokea benchi kunako dakika ya 83 kulijaza pengo la nyota mzawa wa Nigeria, Alex Iwobi ambaye kwa sasa anachezea Everton ya Uingereza.

Mnamo Septemba 19, 2019, alifunga bao na kuchangia magoli mengine mawili katika ushindi wa 3-0 uliosajiliwa na Arsenal dhidi ya Eintracht Frankfurt ya Ujerumani katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi G kwenye kivumbi cha UEFA Europa League msimu huu wa 2019-20.

Asili ya Nigeria

Licha ya kuwa mzaliwa wa Uingereza, Saka ana asili yake nchini Nigeria.

Amewahi kuwa sehemu ya timu ya taifa ya Uingereza kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 16, 17, 18 na 19.

Mnamo Mei 2018, alijumuishwa katika kikosi cha Uingereza kwa makinda wasiozidi umri wa miaka 17 na akawa tegemeo kubwa katika kivumbi cha Euro walichokiandaa.

Licha ya kuwa wenyeji wa pambano hilo, walibanduliwa na Uholanzi katika hatua ya nusu-fainali kupitia penalti hata ingawa yeye binafsi alipachika wavuni mkwaju wake.

Mnamo Septemba 2018, Saka aliwafungia Uingereza bao la ushindi katika kipute cha kirafiki kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 18 dhidi ya Ufaransa.

Ilikuwa hadi Novemba 2018 ambapo alijumuishwa katika kikosi cha Uingereza kwa makinda wasiozidi umri wa miaka 19.

Katika kibarua chake cha kwanza kwenye soka ya kiwango hicho, alicheka na nyavu na hivyo kusaidia timu yake kusajili ushindi wa 3-0 dhidi ya Moldova.

You can share this post!

TAHARIRI: Tatizo si sheria kukabili pombe bali uzingatiaji

DIMBA: Matumaini ya majabali Manchester United kurudia...

adminleo