Kimataifa

Rais apuuza uwezekano wa serikali kupinduliwa

October 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na AFP

BAMAKO, MALI

RAIS wa Mali, Ibrahim Boubacar Keita amepuuzilia mbali madai kwamba kuna njama ya kupindua serikali yake.

Hii ni baada ya uvamizi wa hivi majuzi uliosababisha mauaji ya wanajeshi 38.

Mauaji hayo yalitokea kwenye visa viwili wiki jana karibu na mpaka wa Mali na Burkina Faso.

Hata hivyo, Rais Keita amesisitiza kwamba taifa lake limejifunza kutokana na tukio hilo na linaendelea kuweka mikakati ya kudhibiti hali ya usalama.

“Hakuna mapinduzi yoyote ya jeshi ambayo yatatokea Mali. Nawahakikishia raia wote wa Mali kwamba usalama unaendelea kudumishwa. Sidhani kwamba kuna hofu kwamba jambo kama hilo linaweza kujirudia.” akasema Rais Keita.

Baada ya mauaji ya wanajeshi hao mnamo Jumatatu na Jumanne wiki jana katika miji ya Boulkessy na Mondoro, kiongozi huyo alishikilia kwamba matukio hayo hayafai kulinganishwa na mapinduzi ya jeshi yaliyotokea 2012.

“Uvamizi uliotokea Boulkessy kwa bahati mbaya unaweza kutokea tena na hilo halimaanishi kwamba kuna mapinduzi,” akaongeza.

Wahalifu waliojihami walitumia magari ya kivita kutekeleza mashambulizi hayo kwenye kambi mwili za jeshi kwenye kisa ambacho serikali ilitangaza kuuawa kwa magaidi 15.

Magaidi hao walihepa na bunduki kadhaa na zana nyinginezo za kivita ingawa vyombo vya habari vilitangaza kwamba jeshi lilifaulu kunasa magari 20 pamoja na silaha nyinginezo hatari kutoka kwao.

Duru ziliarifu kwamba wanajeshi wa Mali walisaidiwa na mataifa ya kigeni kama Ufaransa iliyotoa helikopta ya kivita kusaidia kuwafurusha magaidi hao.

Kwingineko, watu sita waliuawa na wengine watano wakajeruhiwa wakati bomu lilipolipuka kwenye eneo linaloshuhudia machafuko ya mara kwa mara kaskazini mwa Mali.

Kulingana na taarifa kutoka la Umoja wa Kimataifa, mjumbe wa amani pia aliuawa karibu na mji wa Aguelhok.

Taarifa hizo zilithibitishwa na Msemaji wa UN nchini Mali, Olivier Salgado.

Mnamo Januari mwaka huu, raia 11 kutoka Chad waliokuwa wanahudumia UN waliuawa na magaidi katika mji wa Aguelhok.

Kundi la kigaidi la Kiislamu la GSIM ambalo linadhaminiwa na Al-Qaeda, lilikiri kutekeleza shambulizi hilo.