Makala

SHINA LA UHAI: Tatizo la shinikizo la damu, aina zake na jinsi ya kudhibiti

October 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 5

Na BENSON MATHEKA

DARIUS Kariuki alianza kuhisi kifua chake kikiwa kizito na akaenda hospitalini.

Alikuwa na miaka 42 na hakuwa amewahi kupata matatizo ya kiafya isipokuwa homa ya hapa na pale au maumivu ya kichwa.

Baada ya kupimwa, daktari alimweleza kwamba alikuwa na msukumo wa damu.

“Nilishtuka kwa sababu sikuwa nimeugua maishani na nilikuwa nikiendelea na shughuli zangu kama kawaida,” asema.

Watu wengi huwa wanashtuka wanapoenda hospitalini na kufahamishwa kwamba wana tatizo la shinikizo la damu maarufu kama Hypertension.

Kulingana na madaktari, shinikizo la damu au presha ya juu ya damu ni ugonjwa ambapo nguvu ya msukumo wa damu katika mishipa ni kubwa kuliko kawaida hivyo husababisha moyo kufanya kazi kupita kiasi ili uzungushe damu katika mishipa ya damu.

Kwa kawaida presha haina dalili ila ikidumu, ina madhara makubwa kwa afya. Mtu husemekana kuwa na presha ikiwa nguvu hizi ni za juu kiasi cha kusababisha matatizo ya kiafya.

Kulingana na shirika la afya ulimwenguni (WHO), ni ugonjwa ambao unaua kimya kimya.

Wataalamu wanasema hupimwa kwa kuchunguza nguvu ya msukumo wa damu katika mishipa ya damu wakati moyo unadunda au umetulia au kati ya mapigo ya moyo.

Moyo unapopiga damu kwa wingi na mishipa ikiwa myembamba, ndivyo msukumo wa damu unavyoongezeka.

Kipimo cha kawaida cha shinikizo la damu ni 100–140 mmHg (kipimo cha juu) na 60–90 mmHg (kipimo cha chini). Shinikizo la juu la damu hutokea kipimo hiki kikiwa zaidi ya 140/90 mmHg kwa muda mrefu.

Dkt Sam Kavoi wa hospitali ya St Lukes mjini Machakos, anasema kinachosababisha hali hii hakijulikani lakini anasema ni hali inayoua watu wengi bila kuonyesha dalili za kuugua.

“Presha ya juu huharibu mishipa na kusababisha maradhi ya moyo isipogunduliwa mapema. Chanzo chake huwa ni kitendawili na sawa na maradhi ya mtindo wa maisha, isiposhughulikiwa inaweza kusababisha matatizo mabaya ya kiafya,” anasema.

Anasema visa vingi vya mshtuko wa moyo na kiharusi vinatokana na msukumo wa damu. Wataalamu wanasema ni hali inayochukua muda mrefu kabla ya kugunduliwa na inakumba karibu kila mtu.

“Habari nzuri ni kuwa ni hali ambayo inaweza kudhibitiwa mtu akifuata ushauri wa daktari na wengi wameishi na hali hii kwa miaka mingi,” asema Dkt Kavoi.

Aidha wanaougua hawana dalili zozote hata kama kiwango hicho ni cha juu mno.

Kulingana na Dkt Kavoi, watu wachache huweza kupata maumivu ya kichwa, kushindwa kupumua au kutokwa na damu puani.

“Hata hivyo, dalili hizi zinaweza kuwa za maradhi mengine na kwa wale walio na presha, hazitokezi hadi kufikia kiwango cha kutishia maisha yao,” aeleza.

Kwa sababu ni hali isiyo na dalili na inayotishia maisha ya wengi, madaktari huwa wanapima kiwango cha msukumo wa damu ambacho wanasema kwa kawaida kinapaswa kuwa 140 kwa 90.

Kulingana na Dkt Robert Ngugi wa hospitali ya Aga Khan, mtu anapaswa kupimwa kiwango cha shinikizo la damu kila baada ya miaka miwili kuanzia umri wa miaka 18.

Anasema jinsi umri unavyoongezeka, ndivyo unakabiliwa na hatari ya kupata presha ya juu.

“Ikiwa una umri wa miaka 40 au zaidi, au ikiwa umri wako ni kati ya 18 na 39 na unakabiliwa na hatari ya kukumbwa na hali hii, pimwa mara mbili kwa mwaka,” aeleza.

Kufanya hivi huwa kunasaidia hali hii kugunduliwa mapema kisha kushauriwa jinsi ya kukabiliana nayo. Kwa kawaida, madaktari huwa wanachunguza kwa muda, kabla ya kutoa ushauri kuhusu jinsi ya kukabiliana nayo endapo itaendelea kutatiza.

“Daktari akigundua kwamba una presha au uko katika hatari ya kupata maradhi ya moyo, hupendekeza upimwe mara kwa mara,” asema.

Utafiti wa shirika BMC Health kwa ushirikiano na wizara ya Afya, mwaka jana ulionyesha kuwa ni asilimia 15.6 ya Wakenya wanaofahamu viwango vyao vya msukumo wa damu na kati ya watu hao ni wachache wanaotibiwa. Utafiti unasema kwa wanaotibiwa, asilimia 51.7 huwa wanapata nafuu.

Kwa sababu unaua kimya kimya bila kuonyesha dalili kwa wengi, wataalamu wanapendekeza watu kupimwa mara mwa mara.

Kulingana na utafiti wa kutathmini hali ya afya wa 2014, ni asilimia 9.4 ya wanawake na asilimia 3 ya wanaume waliotembelea vituo vya afya na kuchunguzwa presha yao.

Takwimu katika ripoti ya WHO, zinaashiria kwamba mwaka wa 2015, watu 1.3 bilioni kote ulimwenguni walikuwa na shinikizo la damu.

Ripoti hiyo inasema kwamba mwanamume mmoja kati ya wanaume 4 ana msukumo wa damu ilhali kati ya wanawake watano, mmoja ana tatizo hilo.

Shirika hilo linalenga kupunguza vifo vinavyosababishwa na msukumo wa damu kwa asilimia 25 kufikia 2025.

Aidha kulingana na WHO, ni vigumu kukadiria wanaouawa na maradhi haya kwa sababu yanasababisha matatizo mengi yanayoua watu. Hata hivyo inakadiria kuwa watu 9.4 milioni hufariki kote ulimwenguni kutokana na matatizo au maradhi yanayosababishwa na msukumo wa damu.

Kadhalika inakisiwa kuwa vifo asilimia 18.4 hadi 32.6 nchini Kenya hutokana na matatizo yanayosababishwa na shinikizo la damu.

Aina za shinikizo la damu

•Primary Hypertension ambayo huwa inachukua muda mrefu kujitokeza.

•Secondary Hypertension ambayo inatokana na sababu nyingine za kiafya.

“Secondary Hypertension huwa inatokea ghafla na kusababisha msukumo wa juu wa damu kuliko Primary Hypertension,” aeleza Dkt Ngugi.

Chanzo cha ‘Secondary Hypertension’:

•Matatizo ya figo

• Matatizo ya tezi kikoromeo

•Matumizi ya dawa kama vile za kupanga uzazi, kutibu homa, kupunguza maumivu.

•Kukosa kupata usingizi

• Kukumbwa na woga.

•Matumizi ya dawa haramu kama kokeni na amphetamines

•Dosari za mishipa ya damu ambazo mtu huzaliwa nazo

Walio katika hatari zaidi ya maambukizi:

•Watu weusi

Wataalamu wanasema Wafrika wanaweza kupata msukumo wa damu wakiwa na umri mdogo kuliko wazungu. Matatizo kama vile kiharusi, mshtuko wa moyo na figo hutokea kwa wingi miongoni mwa Wafrika. WHO inasema asilimia 27 ya watu walio na msukumo wa damu wako Afrika.

• Historia ya familia

Ikiwa unatoka katika familia ambayo kuna watu walio na hali hii, upo hatarini kuugua.

•Unene kupindukia

Jinsi mtu alivyo mnene ndivyo anavyohitaji damu kwa wingi mwilini iweze kusambaza hewa ya oksijeni na virutubishi sehemu zote za mwili. Kiwango cha damu kinapoongezeka kwenye mishipa, ndivyo msukumo unavyoongezeka kwenye mishipa.

•Kuzembea na kukosa kufanya mazoezi

Watu wasiopenda kufanya kazi huwa na moyo unaopiga kwa nguvu. Moyo unapopiga kwa nguvu, ndivyo unavyofanya kazi ili kuweza kuongeza damu mishipani. Aidha, kunafanya mtu kuwa na mwili mnene.

•Uvutaji wa sigara

Matumizi ya tumbako huongeza presha ya damu ghafla japo kwa muda mfupi lakini kemikali katika tumbako zinaweza kuharibu kuta za mishipa. Hii inafanya mishipa kuwa myembamba na kuongeza hatari ya kupata maradhi ya moyo.

•Kutumia chumvi nyingi

•Kupungua kwa madini ya Potassium mwili

Madini ya Potassium (yanayopatikana kwenye matunda kama vile ndizi), husaidia kusawazisha kiwango cha chumvi katika seli.

•Kubugia pombe kwa wingi

Kunywa pombe kwa wingi kwa muda mrefu kunaweza kuharibu moyo. Wataalamu wanasema wanawake wanaokunywa zaidi ya chupa moja kwa siku na wanaume wanaokunywa zaidi ya chupa mbili kwa siku, wanaalika ugonjwa huu.

•Mfadhaiko na msongo wa mawazo

•Baadhi ya maradhi sugu

Baadhi ya maradhi kama vile ya figo, kisukari na kukosa usingizi yanaweza kusababisha msukumo wa damu.

•Mimba

Wajawazito wanapaswa kupimwa mara kwa mara wasiathirike.

•Kula mafuta kwa wingi

Mafuta mwilini hufunga mishipa na kufanya damu kupita kwa shida.

Kulingana na tovuti ya www.medicanewstoday.com, ingawa ni watu wazima wanaokabiliwa na hali hii, watoto wanaweza pia kupatwa na msukumo wa damu hasa walio na matatizo ya figo na moyo. Wazazi wanashauriwa kuwapa watoto lishe bora kuepuka unene kupindukia na kuwasaidia kufanya mazoezi.

Mbali na kusababisha matatizo ya moyo. unaweza kuharibu viungo muhimu vya mwili usiposhughulikiwa.

Matatizo mengine ni kama:

1. Kuvimba tezi.

2. Moyo kusita/kufa

3. Mishipa ya figo kudhoofika

4. Kuathiri mishipa machoni na kusababisha upofu

5. Kuathiri kumbukumbu

Wataalamu wanasema matatizo mengi ya presha ya juu husababisha kifo.

Udhibiti

Shirika la WHO linasema watu wanaweza kupunguza hatari kwa mbinu hizi.

•Punguza kiwango cha chumvi mwilini.

•Kula matunda na mboga kwa wingi

•Kufanya mazoezi

•Kepuka sigara na pombe

•Kutokula mafuta kwa wingi.

•Kuepuka mzongo wa mawazo

•Kupimwa kila wakati

•Kutumia dawa anazopatiwa na daktari na kwa viwango anavyoagizwa.

•Kutibiwa unapougua au kuwa na matatizo viungo vya mwili.

Kulingana na Dkt Kavoi, watu wakianza kutumia dawa za kupunguza msukumo wa damu hawawezi kuacha hadi washauriwe na daktari.

Vilevile, ni hatari kuongeza au kupunguza kiwango cha ulichopewa na daktari.