WaKazi wa Thika wataka huduma kuboreshwa katika ofisi ya ardhi

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Thika wamelalamika vikali kuhusu huduma duni wanayopata katika ofisi ya kushughulikia masuala ya umiliki wa vipande vya ardhi ya Thika, wakitaka irekebishwe.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alilazimika kuingilia kati ili kuona ya kwamba mambo yanakwenda sawa.

Alisema kwa muda mrefu watu wengi wamempigia simu hata kufika ofisini mwake na kutoa malalamishi kuhusu jinsi hakuna huduma ya kuridhisha inayotolewa katika ofisi hiyo.

“Ilibidi nijiwasilishe mwenyewe katika ofisi ya ardhi ili nielewa hasa kiini cha malalamiko hayo ambayo yameendelea kwa muda mrefu sasa,” alisema Bw Wainaina.

Alisema baada ya kuketi chini kwa majadiliano na afisa mkuu wa ardhi (Registrar), Bw Benard Leitich, aliarifiwa ya kwamba kuna ukosefu wa wafanyakazi ambapo kuna 20 pekee ambapo idadi kamili ya kutosheleza huduma hiyo ni 35 kulingana na afisa huyo.

Alisema wananchi wengi wanatoka sehemu za Murang’a, na Machakos, ili kufanya ‘search’ ya kutafuta hatimiliki.

Kutokana na malalamiko hayo, alisema atalazimika kukutana na Waziri wa Ardhi Bi Faridah Karoney ili kutatua jambo hilo ambalo limekuwa kero kubwa katika ofisi hiyo ya ardhi.

“Nitafanya juhudi kuona ya kwamba ofisi hii inahudumia watu bila ubaguzi wowote na ningetaka kuona pia kila mwananchi anahudumiwa kwa haki,” alisema Bw Wainaina.

Akaongeza: “Ninaelewa vyema kuna mawakala ambao kazi yao kubwa huwa ni kusimama nje ya ofisi ya ardhi wakiwahadaa watu hasa wakongwe, eti watawasaidia kupata hatimiliki,” alisema mbunge huyo.

Alisema kwa vile wanakosa hata magari ya kutumia kuenda sehemu za mbali, amekubali kutoa mara moja kwa wiki gari la Landrover la hazina ya CDF kuisaidia idara hiyo.

Wakazi wa Thika waliridhishwa na mbunge wao ambaye aliingilia kati shida zao za ardhi kwa haraka.

Afisa mkuu wa ardhi katika Thika Bw Benard Leitich alisema upungufu wa wafanyakazi imekuwa ni kizingiti kikubwa kinachoponza juhudi zao kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

“Kwa sasa nina wafanyakazi 20 pekee ambao wanaendesha kazi hiyo nzito na ninahitaji wafanyakazi 35 kwa jumla ili kazi ifanyike vilivyo,” alisema Bw Leitich.

Habari zinazohusiana na hii