Habari Mseto

Wazee sasa kuweka viwango vya mahari

October 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WANYORO

BARAZA la Wazee wa Jamii ya Ameru la Njuri Ncheke limetangaza mipango ya kusawazisha mahari yanayotolewa kwa familia za wanawake katika jamii yao ili kuhimiza vijana kuoa.

Katibu Mkuu wa baraza hilo, Bw Josephat Murangiri alisema wanandoa wengi hawafurahii ndoa zao kwa sababu ya mahitaji ya mahari.

Akizungumza katika makao makuu ya Kaunti ya Meru wakati wa kutia sahihi makubaliano ya pamoja kati ya kaunti na idara ya kitaifa ya kusimamia makavazi kuhusu ujenzi wa makavazi itakayogharimu Sh50 milioni, Bw Murungari alisema wazee watakutana hivi karibuni kujadili suala hilo.

Alisema wamegundua kwamba ugomvi wa kinyumbani husababishwa zaidi na jinsi wanandoa hawana furaha baada ya kushindwa kuoa wapenzi wao wa zamani kwa vile hawakuweza kuwalipia mahari.

“Ndoa si biashara kwamba aliye na uwezo wa kifedha ndiye anayemchukua binti, hata kama hawajapendana. Enzi za mababu zetu ambapo watu walifungishwa ndoa kisha wakapendana wakiwa wanaishi pamoja zimepitwa na wakati. Kuna haja ya kuweka mazingira ambapo mvulana na msichana wakipendana, watakuwa na uwezo wa kuoana,” akasema.

Bw Murangiri alisema baraza hilo linaunga mkono pendekezo la Gavana Kiraitu Murungi kusawazisha kiwango cha mahari kinachostahili kutolewa. Gavana huyo alikuwa ameeleza masikitiko yake kuhusu jinsi kuna watu wanaoitisha hata Sh1 milioni kutoka kwa vijana wanaotaka kuoa binti zao.

“Mababu wetu walikuwa na nia ya kuona kuwa kila mtu anaishi maisha ya furaha. Ugomvi mwingi wa kinyumbani hutokea kwa vile watu wengi wameoana ilhali si wapenzi. Tutakutana ili kuweka kiwango kimoja cha mahari lakini kama mtu atataka kulipa zaidi, basi yuko huru,” akasema Bw Murangiri.

Makavazi

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na mkurugenzi wa idara ya kitaifa ya makavazi, Dkt Mzalendo Kibunjia.

Katika jamii nyingi za Kibantu, mahari kitamaduni huhusisha mbuzi, kondoo au kuku pamoja na pombe. Wazee hupokea kibuyu cha pombe na mama hupewa kikoi au nguo kuashiria nguo aliyotumia kubeba binti. Kisha watu hupika chakula na kula pamoja, ishara ya kuunganisha familia mbili.

Lakini kuingia kwa utamaduni wa Magharibi kumegeuza mambo, ambapo sasa mahari hutozwa kutegemea gharama ya wazazi kumlea binti, ikijumuisha hadi karo ya hadi Chuo Kikuu.