Kocha wa Gor: Siwezi kugura kikosi kikiwa sasa ndio kimeiva
Na CECIL ODONGO
MKUFUNZI wa klabu ya Gor Mahia, Steven Polack, amekanusha uvumi unaoenea kwamba amegura timu hiyo, akisema ameenda likizo ya wiki moja nchini Finland.
Polack raia wa Uingereza aliwaondolea mashabiki wa timu hiyo hofu, akisema ameenda kujivinjari na familia yake na atarajea Jumapili kuendelea kunoa timu hiyo. Mkufunzi huyo ambaye aliondoka nchini Jumatatu jioni pia ana uraia wa Finland.
Kumeibuka madai kwamba Polack huenda asirejee nchini kama tu mtangulizi wake Hassan Oktay ambaye aliyoyomea kwao Uturuki kisha akajiuzulu wadhifa wake mwezi Agosti akiwa huko.
Alisema aliamua kuenda likizo kipindi hiki ambapo kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani(FIFA) limepisha mechi kadhaa za kimataifa zinazoanza leo hadi Jumapili ili kujumuika na familia na marafikize.
“Mimi ni mtu mwadilifu tena mpenda ukweli. Nitatii na kuheshimu mkataba wa miaka miwili ambao niliusaini na Gor Mahia mwezi Agosti. Kwa nini niondoke ilhali kikosi sasa kimeiva na klabu ipo kileleni mwa jedwali?,” akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo.
Kipindi kifupi
Aidha alitaja kushangazwa kwake na habari za kutoroka timu hiyo, akishikilia hayupo kwenye orodha ya makocha ambao hugura klabu baada ya kuhudumu tu kwa kipindi kifupi.
“Rafiki yangu kutoka Ghana amenipigia simu baada ya kupokea habari feki kwamba nimeacha kazi ya ukufunzi Gor Mahia. Nimemweleza nipo likizoni hadi Jumapili na nitaendelea na kazi yangu nikirudi. Wanaoeneza habari hizo wanafaa wakome kwa kuwa mimi bado ni kocha wa Gor Mahia,” akaongeza.
Vilevile alikiri kwamba amelipwa mshahara wake na mabingwa hao mara 18 wa Ligi Kuu(KPL), habari ambazo pia zilithibitishwa na Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Mahia Lordvick Aduda.