• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
Ruweida Obbo sasa ataka wapigambizi wa Lamu kushirikishwa katika uopoaji wa miili

Ruweida Obbo sasa ataka wapigambizi wa Lamu kushirikishwa katika uopoaji wa miili

Na KALUME KAZUNGU

MWAKILISHI wa Wanawake wa Kaunti ya Lamu katika Bunge la Kitaifa Bi Ruweida Obbo ameitaka serikali kuwashirikisha wapigambizi wa kujitolea kutoka Lamu katika operesheni ambayo inaendelea ya kutafuta miili ya mama na mwanawe waliozama kwenye Bahari Hindi katika kuvuko cha Likoni, Kaunti ya Mombasa.

Bi Mariam Kighenda na mwanawe Amanda Mutheu walikumbana na balaa gari lao lilipodondoka kutoka kwa feri na kutumbukia baharini Septemba 29, 2019, katika kivuko hicho cha Likoni.

Aidha juhudi za wanamaji wa Kenya na pia wapigambizi – wa hapa nchini na wengine kutoka nje – za kujaribu kuopoa miili baharini hazijazaa matunda kufikia sasa ingawa imeelezwa kwamba wamepata vifaa vya kisasa.

Katika mahojiano na wanahabari mjini Lamu, Bi Obbo alishikilia kuwa kuna haja ya serikali kuwazingatia wapigambizi kutoka Kaunti ya Lamu ambao alisema wengi wao wana tajiriba ya muda mrefu.

Mwakilishi huyo wa wanawake alisema anaamini kushirikishwa kwa wapigambizi wa Lamu kwenye shughuli za uopoaji wa miili kwenye kivuko cha Likoni huenda kukabadili hali na kupelekea miili hiyo kupatikana.

Alisema wapigambizi wa Lamu wako na kipawa katika kazi hiyo.

Alisema cha kutia moyo zaidi ni kwamba wapigambizi wa Lamu tayari wamehusika katika shughuli za kuokoa na hata kuopoa miili ya wale ambao wamekuwa wakizama baharini wakati ajali za boti na mashaua zinatokea eneo hilo.

Boti kuzama

Mnamo Agosti 13, 2017, watu 12 wa familia ya mwanasiasa, Shekuwe Kahale waliangamia baharini eneo la Manda Bruno baada ya boti yao kukumbwa na mawimbi na dhoruba kali baharini na kuzama.

Ni mwanasiasa Kahale pekee ndiye aliyenusurika kifo baada ya kuogelea hadi nchi kavu.

Aidha shughuli ya kuopoa miili ya walioangamia ilitekelezwa na wapigambizi wa kujitolea wa Lamu.

“Sielewi ni kwa nini serikali inasahau kwamba Lamu tuna watu wa tajiriba ya juu katika masuala haya ya kupiga mbizi na kutafuta walioangamia baharini. Vijana wetu wako tele na wana uzoefu wao wa bahari hapa Lamu. Kwa nini serikali isiwashirikishe katika shughuli za uopoaji kule Likoni? Ninaamini vijana wa Lamu wakishirikishwa kutakuwa na mabadiliko makubwa na hata miili huenda ikapatikana upesi,” akasema Bi Obbo.

Mbunge huyo aidha aliikashifu serikali kwa kufeli kuwaajiri watu wa tajiriba ya masuala ya baharini eneo la Likoni Feri.

“Haya masuala ya bahari ni heri yaachiwe watu wa eneo hili la Pwani ambao wana uzoefu tele. Inashangaza kwamba wanaoajiriwa hasa pale Likoni Feri ni watu ambao wengi wao hawana uzoefu wa bahari. Hii ndiyo sababu hata uopoaji wa miili hawaiwezi. Ombi langu ni kwamba serikali ifikirie kuajiri watu wa tajiriba kulingana na Nyanja husika,” akasema Bi Obbo.

You can share this post!

Uopoaji: Wapigambizi sasa kuweka zingatio kwa sehemu ya...

KINA CHA FIKIRA: Sawa na Kiingereza, kuna Kiswahili na...

adminleo