Habari Mseto

Sikukuu yaendelea kumjenga Mzee Moi

October 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na WANDERI KAMAU

HATUA ya Serikali kuendeleza sherehe za Moi Dei inatimiza ndoto ya Rais mstaafu Daniel Moi kuendelea kukumbukwa hata baada ya kuondoka madarakani.

Sikukuu hii ilikuwa ikisherehekewa na Wakenya kuanzia 1988 kuadhimisha Mzee Moi kuchukua mamlaka kutoka kwa Mzee Jomo Kenyatta mnamo 1978. Alitaka kuwe na siku ya kumkumbuka sawa na mtangulizi wake alivyokuwa na sikukuu iliyoitanishwa naye

Hata hivyo, ilifutiliwa mbali na Katiba ya sasa mnamo 2010 kwa msingi kuwa kuadhimishwa kwake hakukuwa na umuhimu wa historia ya nchi.

Lakini mnamo 2017, Mahakama Kuu ya Nairobi iliagiza kuwa siku hiyo ni sikukuu ya umma, hivyo inapaswa kurejeshwa miongoni mwa sikukuu za kitaifa zinazoadhimishwa rasmi.

Wachanganuzi wanasema kuwa kuendelea kuadhimishwa kwa Moi Dei kunamjenga Mzee Moi, licha yake kutokuwa kwenye ulingo wa kisiasa.

“Hatua ya kuendelea kuadhimisha sikukuu hii inamjenga Mzee Moi, kwani inamaanisha kuwa jina lake litaendelea kuwa vinywani mwa Wakenya, licha yake kutokuwa uongozini,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya siasa.

Tangu mwaka 2018 Mzee Moi amekuwa akipokea jumbe za viongozi mbalimbali wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, ambaye amemtembelea mara kadhaa nyumbani kwake katika eneo la Kabarak, Kaunti ya Nakuru.

Mzee Moi amehusishwa na siasa za 2022, ambapo mwanawe Seneta Gideon Moi wa Baringo ametangaza huenda akawania urais.

“Sikukuu hii inaashiria umuhimu mkubwa wa kisiasa alio nao Mzee Moi,” asema Prof Munene.