• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
Mshukiwa wa mauaji apinga video kuonyeshwa kortini

Mshukiwa wa mauaji apinga video kuonyeshwa kortini

Na RICHARD MUNGUTI

MSHUKIWA wa mauaji ya wakili Willie Kimani, mteja wake na dereva wa teksi Jumatano alipinga vikali kuchezwa kwa video iliyorekodiwa eneo walikouawa kinyama watatu hao mahakamani.

Katika video hiyo, Peter Ngugi Kamau, aliyekuwa ameorodheshwa na idara ya polisi mpashaji habari za matukio ya uhalifu, alirekodiwa akiwaonyesha kundi la maafisa wa polisi waliochunguza mauaji ya watatu hao eneo la mauaji, utekaji nyara na mahala walikotupa maiti zao mtoni Athi River, Donyo Sabuk , kaunti ya Machakos.

Wakili Kelvin Michuki, anayemwakilisha Ngugi, alimweleza Jaji Jessie Lesiit, anayesikiza kesi hiyo kwamba , video hiyo itaathiri vibaya kesi inayomkabili.

“Kwa mujibu wa Kifungu nambari 50 cha Katiba, washukiwa wamekatazwa kuwapa polisi ushahidi utakaotumika kuthibitisha kesi inayowakabili,” Bw Michuki alimweleza Jaji Lesiit.

Wakili huyo alisema sheria iwazi kwamba maungamo ya mshukiwa yeyote nje ya mahakama hayapasi kutegemewa kama ushahidi katika kesi inayomkabili.

Bw Michuki alisema kifungu nambari 25 (a) cha sheria za maungamo zimeeleza utaratibu wa mshukiwa kufichua anayojua ama alichofanya kabla ya kutiwa nguvuni na kushtakiwa.

“Kulingana na kifungu nambari 6 (2) cha ushahidi, mshukiwa anapasa kuonywa kuhusu maungamo yake na kuonywa ipasavyo kabla ya kutoboa siri,” alisema Bw Michuki.

Wakili huyo alipinga kuchezwa kwa video hiyo kortini na afisa wa polisi Joseph Muindi, aliyeichukua.

“Ijapokuwa video hii ilichukuliwa na mtu asiyehusika na uchunguzi wa kesi hii inamuhusu Ngugi na jinsi alivyohusika katika mauaji hayo. Ni ushahidi wa maungamo yake na haupaswi kukubaliwa,” alisema Bw Michuki.

“Mshtakiwa hakuonywa ipasavyo kisheria. Alitaka achukuliwe video akielezwa vile sheria hutaka kwa anayeungama alichotenda ama alishuhudia kikitekelezwa,” Bw Michuki alimweleza Jaji Lesiit.

Mahakama iliambiwa Bw Muindi na afisa anayechunguza kesi hiyo Inspekta Mkuu Clement Mwangi walikaidi sheria na “kwamba video iliyochukuliwa maeneo ya mauaji na kwingineko yapasa kukataliwa.”

Lakini kiongozi wa mashtaka Nicholas Mutuku aliomba mahakama imruhusu Bw Muindi kuonyesha video aliyochukua eneo la mauaji, kituo cha polisi wa utawala cha Mlolongo, Mahakama ya Mavoko, kivuko cha reli mjini Athi River, Kwambira (Limuru) ambapo gari la teksi iliachwa na Donyo Sabuk ambapo maiti za Willy Kimani, Josephert Mwenda na Joseph Muiruri zilitupwa.

Maiti hizo zilipatikana baada ya wiki moja zikiwa zimeoza.

Bw Mutuku alimweleza Jaji Lesiit kwamba hakuna sheria ilikiukwa na mshtakiwa alielezwa kile alihitajika kujua kisheria kabla ya kupeleka polisi mahala kwote uko.

Jaji Lesiit atatoa uamuzi ikiwa atakubali video hiyo ichezwe au la mnamo Oktoba 14, 2019.

Kamau ameshtakiwa pamoja na waliokuwa polisi wa utawala Inspekta Fredrick Leliman, Stephen Cheburet, Sylvia Wanjiku na Sajini Leonard Maina Mwangi aliwaongoza maafisa wa polisi kuchukua picha za video mnamo Agosti 10, 2016.

You can share this post!

Sikukuu yaendelea kumjenga Mzee Moi

Shirika la Posta kufanyiwa mageuzi ili kuendana na...

adminleo