• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Watu 55 wanusurika kwenye ajali ya ndege uwanjani Wilson

Watu 55 wanusurika kwenye ajali ya ndege uwanjani Wilson

Na MARY WANGARI

RAIS Uhuru Kenyatta amepongeza makundi ya uokoaji kwa hatua ya haraka kufuatia kisa ambapo watu 55 wakiwemo abiria 50 na wahudumu watano wa ndege walinusurika kifo baada ya ndege waliyokuwemo ndani kuteleza Ijumaa ilipokuwa ikianza kupaa.

Taharuki ilitanda Ijumaa asubuhi wakati ndege hiyo aina ya Fokker 50, 5Y-IZO, ya shirika la Silverstone Air, iliyokuwa ikielekea Lamu kutoka Nairobi, ilipokosa mwelekeo wakati wa kupaa jana saa tatu asubuhi, ambapo watu wawili walijeruhiwa.

“Rais Uhuru Kenyatta anapongeza timu za uokoaji katika Uwanja wa Ndege wa Wilson Nairobi kwa hatua yao ya haraka kufuatia ajali iliyohusisha ndege ya Fokker 50 ya shirika la Silverstone Air. Rais pia anawatakia afueni ya haraka abiria waliojeruhiwa katika kisa hicho,” alisema Uhuru kupitia taarifa.

Ikithibitisha kisa hicho, kampuni ya Silverstone Air vilevile iliwashukuru maafisa wa idara ya dharura katika Uwanja wa Ndege wa Wilson kwa hatua yao ya haraka iliyowezesha abiria wote kutolewa wakiwa salama.

“Tunaweza kuthibitisha kwamba ndege yetu aina ya Fokker 50, 5Y-IZO imekumbwa na kisa ilipokuwa ikipaa katika Uwanja wa Ndege wa Wilson saa tatu leo (Ijumaa) asubuhi. Ndege hiyo ilikuwa ikitumia mkondo wa Wilson-Mombasa-Lamu-Mombasa-Wilson. Abiria na wahudumu wametolewa salama na kwa sasa tunashirikiana na mamlaka husika kutathmini hali. Tunashukuru huduma za dharura katika Uwanja wa Ndege wa Wilson kwa hatua yao ya haraka na ushirikiano,” ilisema Silverstone Air kupitia taarifa.

Kulingana na Mamlaka ya Usafiri wa Ndege (KAA), abiria wawili walipata majeraha madogo huku ikisema kwamba uchunguzi ulikuwa ukifanywa ili kubaini kiini cha ajali hiyo.

“Asubuhi ya leo (Ijumaa) mwendo wa saa tatu asubuhi, ndege aina ya Fokker 50 yenye nambari ya usajili 5Y-IZO ya shirika la Silverstone Air ilipotea mwelekeo kwenye mkondo ilipokuwa ikipaa katika Uwanja wa Ndege wa Wilson, Nairobi. Ndege hiyo ilikuwa na watu 55, abiria 50 na wahudumu watano. Abiria wawili walijeruhiwa kidogo na wanapokea matibabu yanayofaa. Idara ya Uchunguzi wa Ajali za Ndege katika Wizara ya Usafiri na Miundomsingi inafanya uchunguzi kubaini kiini cha ajali hiyo,” ilisema KAA kupitia taarifa.

Ndege ya Fokker 50 iliyohusika katika kisa hicho ni miongoni mwa ndege zisizopungua 10 zinazomilikiwa na Siverstone Air, inayoendesha shughuli zake za usafiri katika maeneo sita Kenya ikiwemo: Kisumu, Lodwar, Malindi, Lamu, Mombasa na Ukunda.

Wakenya pia walijitosa mitandaoni kupongeza maafisa wa kukabiliana na dharura katika Uwanja huo wakihoji kwamba hali ingekuwa hivyo kote nchini baadhi ya visa kama vile mkasa wa Feri ya Likoni, vingeweza kuzuiwa.

You can share this post!

DAU LA MAISHA: Ni mpasuaji pekee wa kike wa kansa ya titi

Hatimaye gari na miili ya mwanamke na bintiye yaondolewa...

adminleo