• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 6:55 PM
TAHARIRI: Afaulu asifaulu leo Kipchoge asalia shujaa

TAHARIRI: Afaulu asifaulu leo Kipchoge asalia shujaa

Na MHARIRI

LEO ni siku kuu duniani.

Ni siku muhimu kwa sababu yupo mwanadamu ambaye anathubutu kuweka historia ambapo akifaulu atakumbukwa milele.

Umaalumu wa siku ya leo unatokana na juhudi za mtoto mwenye asili ya Kenya. Mkenya hasa!

Ni mwanamume ambaye amefanya uamuzi mgumu wa kujaribu kile ambacho hakuna binadamu katika historia ya mbio za nyika amewahi kufanya.

Eliud Kipchoge amefanya mazoezi makali kwa miezi kadha sasa.

Amejinyima mengi katika haya mazoezi ya kuanzia kila Alfajiri.

Hamasa iliyomwongoza katika muda huu wote ni ile kauli mbiu ya mbio hizi kwamba ‘Binadamu ana uwezo wa kuafikia chochote kile anachokiwania.’

Zaidi ya haya kwa wale wanaomjua Kipchoge kwa karibu wataungama kwa yeye ni miongoni mwa wanamichezo wastaarabu ajabu ambao taifa hili limewahi kujaliwa. Amejawa utu na siku zote hupenda kuwa kielelezo kwa chipukizi katika jamii.

Aidha, yeye daima hutambua mchango ambao Mungu amemjalia katika maisha yake na hivyo kuchangia ufanisi.

Ni kutokana na sifa hizi tumbi nzima ndipo mashirika mabalimbal;i yamejitokeza kuwa mshirika wake. Muhimu zaidi duniani ni Kampuni ya INEOS ambayo kwa kutambua juhudi za gwiji huyu, katika busara yake iliamua kuandaa mbio hizi za nyika za aina yake kuwahi kuandaliwa duniani kwa nia ya kumpa mazingira bora zaidi ya kumwezesha kuvunja rekodi yake ya sasa aliyoiweka katika makala yaliyopita ya mbio za berlin Marathon.

Nchini Kenya kampuni ya mawasiliano ya Safaricom imefanya uamuzi wa kihistoria; kwamba jina na nembo ya M-Pesa kwa muda wa siku saba sasa itakuwa jina la kwanza la Kipchoge yaani ELIUD.

Hii ni staha kubwa sana ambayo wengi tunatumaini kwamba itakuwa kichocheo kitakachomshajiisha katika mbio za leo.

Wakenya kupitia kwa mitandao mbalimbali ya kijamii pia wamemtumia Kipchoge lukuki ya jumbe za heri jagina huyu kumtia moyo.

Tunamtakia kila la kheri Kipchoge anapojitosa uwanjani akisaidiwa na wakimbiaji wa mbio mbalimbali kutoka kote duniani kwa azma ya kumsaidia kuvunja rekodi yake.

Ni muhimu kusisitiza kwamba Kipchoge ashinde au asishinde atasalia kuwa shujaa nchini Kenya na Duniani kote.

Hata hivyo, ni maombi ya wengi wetu kwamba Kipchoge ataibuka mshindi ili kuwezesha wote wenye ndoto mbalimbali maishani kuamini kwamba inawezekana kuafikia matamanio yoyote waliyonayo wakiwa na nia ya dhati.

You can share this post!

UMBEA: Maisha ya ndoa yapo katika hatua 3: Raha, ujana na...

MWANAMKE MWELEDI: Mtangazaji mahiri si hapa nyumbani tu!

adminleo