• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:55 PM
MWANAMUME KAMILI: Tunaishi katika ulimwengu wa wanadamu vigeugeu wanaovuta kamba kwao huku wakitafuta kila njia wenzao kuwatokomeza!

MWANAMUME KAMILI: Tunaishi katika ulimwengu wa wanadamu vigeugeu wanaovuta kamba kwao huku wakitafuta kila njia wenzao kuwatokomeza!

Na DKT CHARLES OBENE

NINAKUMBUKA kaulimbiu ya chama kimoja cha kisiasa kilichoasisi na kushawishi wanachama kwenda mbele.

“Mbele Pamoja” bila shaka ilinuiwa kuchochea hamasa na kuwapa motisha waliounga mkono chama kile kwenda mbele.

Ukweli dhahiri shahiri ni kwamba kila mtu analenga kusonga hatua mbele japo chache. Si kimaisha, si kitaaluma, si kifedha si kiroho, si kimaadili, si kifamilia na vigezo vinginevyo!

Ndivyo, kila mmoja analenga kwenda mbele licha ya kwamba baadhi yetu tunaishi bila mbele wala nyuma kwa maana halisi ya “mbele” na “nyuma!” Wajua tena tulivyo vigeugeu mambo kuyabadili kwa manufaa yetu binafsi.

Kama mumunye, tumekwisha haribikia udogoni tukajua maana mbadala ya “mbele” na “nyuma!” Hayo ni yenu nyie wajuvi wa mambo na vijimambo vya dunia!

Pongezi kwa wanawake na wanaume wanaojitahidi kusonga mbele pamoja. Hivyo ndivyo wanavyofanya watu wazima wenye akili timamu. Hongera kwa zenu jitihada. Chudi na bidii wanazotia waja katika shughuli za kila siku zinalenga kutimiza shabaha ya “kusonga hatua mbele!”

Hata hivyo inavunja moyo kuona jinsi wanadamu wachache walivyozembea kiasi kwamba wanarudisha nyuma gurudumu la wengi walioradhi “kwenda mbele!” Kuna wanaume kwa wanawake walioteuliwa ama waliojitwika wadhifa wa kuongoza wenzao katika safari ya “kwenda mbele” ambao sasa wamekuwa vizingiti katika safari hiyo ya kwenda mbele.

Kile kisa cha mama na mwanawe kuzama majini kwenye kivukio cha Likoni Kaunti ya Mombasa ni ishara tosha kwamba kuna watu na viatu! Vipi tunavyoweza kuishi majini ilhali hatuna wanaume kwa wanawake wanaoweza piga mbizi wakati wa dharura? Jeshi zima la Wanamaji wako hatua chache kutoka kivukio kile lakini hapakuwa na hata mmoja aliyefika kwa msaada wa dharura. Badala ya uokozi, tuliona heri kupiga picha, kurekodi video na kutundika mitandaoni! Ama kweli tunaenda “mbele pamoja!”

Ni jambo la kuhuzunisha mno kuwaona wanasiasa walioasisi kaulimbiu ya kwenda “mbele pamoja” wakifarakana na kuzozania uongozi na mamlaka badala ya kutendea wema walalahoi wanaohitaji huduma za serikali.

Na sio migogoro pekee inayotuvunja moyo. Viongozi walioahidi safari ya “mbele pamoja” ndio kwanza wametajwa katika kashfa za uporaji mali ya umma na uharibifu wa miundomsingi nchini.

Vipi taifa litasonga mbele ikiwa semi za wanaume kwa wanawake wa leo ni tofauti mno na vitendo vyao? Mbona iwe rahisi kwetu wanadamu kusema moja na kutenda tofauti mno na ahadi zetu?

Kila ninaposikiliza ahadi wanazotoa maharusi maabadani, mahafala vyuoni, wanasiasa bungeni, wanenguaji unyagoni ama hata wachawi kilingeni, ninaona mwanga kwamba safari ya “mbele pamoja” sio ndoto!

Ukweli ni kwamba tuemesalia katika ndoto kukumbatia mapapo na shauku tu ila hatujasonga hatua moja mbele. Maharusi wanaanzia vita vyao wangali kwenye fungate.

Kesi za talaka ni nyingi mahakamani kuliko zile za uhalifu! Vipi jamii zetu zitasonga mbele pomoja katika hali ya chuki na uhasama?

Mara ngapi tumesikia visa vya mauaji na maangamizi nyumbani vinavyotekelezwa na watu wazima walioahidi safari ya “mbele pamoja?”

Kisa cha mwanamume kumteketeza mkewe kwa mafuta ya taa katika Kaunti ya Nakuru kinatukumbusha tu kwamba wanadamu walikwisha asi utu kitambo.

Mwanamume yule alikwisha sahau kabisa ahadi zote na nakshi za maisha alizotumia kama chambo kumnsa mwanamtu. Amekwisha vilevile kumzalisha na kumnyonyoa kuku bila maji ndio maana anaona heri mwili wa mtu kuuchanja kwa mafuta ya taa. Hao ndio wanaume tunaotegemea katika safari ya “mbele pamoja!”

Jamani wapi usawa katika dunia hii ambamo watu wanatumbuana usaha badala ya kwenda mbele pamoja? Nilidhani kwamba tumekwisha zika fikra na mawazo duni za waja kumalizana mchana wa jua. Nilidhani tuko ndani ya utandawazi – dunia inayozingatia haki, tena inayoheshimu mchango wa kila mmoja katika jamii. Nilidhani tunaishi katika dunia ya usawa japo sijui kasawazisha nani! Nimesalia na dhana tu!

Tunaishi katika dunia ya wanadamu vigeugeu wanaovuta kamba kwao huku wakitafuta kila njia wenzao kuwatokomeza! Ndio maana wanawake wameasi msamaha kwenye familia wakaona heri kuanika mambo kwenya mahakama kila mmoja akipigania “mgao wa mali”. Wanawake kwa wanaume wa leo wameacha kabisa kufuata mkondo wa “mbele pamoja.” Kila mmoja anaona heri kwenda njia yake na mali yake. Tumesalia tu wanadamu wanaotafuta kivuli cha muda kusubiri wenzetu kuchuma kwa jasho lao kabla kivumbi kutifuka chumbani na mambo kufika meza ya mahakama.

Ukweli ni kwamba lau tamaa ya mali na uzembe wa baadhi ya wanawake kwa wanaume wa leo safari ya mbele pamoja ingaliafikiwa na mili na roho zetu kutulia; sote tukiwa jamii na taifa linalolenga mbele pamoja! Hayo ndio mawazo na fikra za mwanamume kamili!

 

[email protected]

You can share this post!

Hatimaye gari na miili ya mwanamke na bintiye yaondolewa...

INEOS 1:59 Challenge: Eliud Kipchoge afaulu kukamilisha...

adminleo