DAU LA MAISHA: Ni mpasuaji pekee wa kike wa kansa ya titi
Na PAULINE ONGAJI
KATIKA taaluma inayotawaliwa na wanaume, amejijenga himaya kubwa si haba.
Kutana na Dkt Miriam Mutebi, mpasuaji pekee wa kike wa kansa ya matiti humu nchini, na Naibu Profesa katika Chuo Kikuu cha Aga Khan.
Huu ukiwa mwaka wake wa nne katika taaluma hii, Dkt Mutebi ni mmojawapo wa wataalamu wachache katika nyanja hii humu nchini wanaotoa matumaini kwa maelfu ya wanawake na hata wanaume wanaokumbwa na maradhi haya.
Kwa usaidizi wa wataalamu wengine wanaohusika na maradhi haya, kazi yake inahusisha kutambua maradhi ya kansa, kuchagua mbinu mwafaka zinazomfaa mgonjwa na baadaye kutoa tiba ambapo hasa anahusika na kitengo cha upasuaji.
“Kazi yangu haihusishi tu kuondoa seli za kansa au titi lililoathirika kwa njia ya upasuaji, kwa kutumia teknolojia mpya sasa pia tunaweza hifadhi ngozi ya mhusika na hata wakati mwingine chuchu zake zitakazotumika kumuundia titi mpya baada ya lililoathirika kuondolewa. Hii ni afueni kwa sababu inasaidia wanawake kudumisha umbo lao la kawaida, na hivyo kuwaongezea hisia za kujithamini,” aeleza.
Lakini mbali na masuala ya kimatibabu, anaelimisha na kuhamasisha watu kuhusu maradhi haya, vile vile kuwapa moyo wale wanaogua. Na kazi yake imetambulika humu nchini na kimataifa. Hivi majuzi alitambuliwa kama mwanachama wa Muungano wa udhibiti wa kansa kimataifa (UICC).
Lakini haijakuwa rahisi kwa Dkt Mutebi. “Ni kazi ambayo mara nyingi inakukutanisha ana kwa ana na mauti, na hasa changamoto ya kujulisha jamaa zao, suala ambalo huleta majonzi,” aeleza.
Lakini licha ya hayo, anasema kwamba ni kazi ambayo lazima ifanywe kwani inaokoa maisha, na wazo hilo humpa moyo kuendelea. “Mara nyingi kama wataalamu, sisi huwa na vikao ambapo sote huzungumza, kujadiliana na kupeana nguvu za kuendelea na kazi hii,” aeleza.
Pia, kuna changamoto ya uchovu unaotokana na kuhudumia idadi kubwa ya wagonjwa.
“Kwa mwezi tunaweza kuhudumia kati ya wagonjwa 30 na 40 wa kansa ya matiti ambapo tatizo la kila mmoja huwa tofauti na kushughulikiwa kuambatana na mahitaji yake. Hii sio rahisi kwani huchukua nguvu na wakati mwingi hasa ikizingatiwa kwamba wataalamu ni wachache,” aeleza, huku akiongeza kwamba ari ya kutaka kuhudumia wagonjwa imekuwa ikimpa nguvu kila wakati.
Mbali na hayo, anasema kwamba kuwa mtaalamu wa kike katika taaluma inayotawaliwa na wanaume, pia kumekuwa na changamoto zake. “Sio kwamba nimekuwa nikitengwa au kubaguliwa. Wenzangu wa kiume wamenichukua kama mmoja wao. Hata hivyo, maradhi ya kansa ya matiti huathiri sana wanawake ambapo nahisi kwamba ingekuwa vyema iwapo kungekuwa na uwakilishi zaidi wa wanawake,” aeleza.
Dkt Mutebi ambaye ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Chuo Kikuu cha Cape Town, Afrika Kusini, na Chuo Kikuu cha Weill Cornell, Amerika, anasema kwamba azma yake hasa ya kujihusisha na kansa ya matiti ilimjia akiwa katika chuo kikuu.
“Kama sehemu ya kozi (rotation) chuoni, nilijipata nikitumia muda mwingi katika kliniki ya kansa ya matiti. Muda ulivyokuwa ukisonga tulikumbana na visa vingi hasa miongoni mwa mabibi barubaru, ikilinganishwa na wanawake waliokomaa kiumri. Hii ilinichochea kujua zaidi? Na ni hapa nilikata kauli,” aeleza.
Anasema kwamba ukosefu wa ufahamu wa kutosha umeonekana kuchangia ongezeko la idadi ya vifo kutokana na maradhi haya, na hii ni mojawapo ya sababu ambazo zimemfanya kuhusika pakubwa katika kampeni za uhamasishaji.
Ushauri wake kwa wasichana ambao wangependa kujihusisha na taaluma hii ni kufuata ndoto zao na kuwa wakakamavu na wenye bidii.
“Unapaswa kuhakikisha kwamba unatumia vyema kila fursa unayokumbana nayo. Aidha, ni vyema kutafuta wanasihi hasa katika taaluma hii, watakaokupa mwongozo na kukusaidia kupata taswira kamili ya tasnia hii,” aeleza.
Pamoja na wenzake, wameanzisha Pan-African Women’s Association of Surgeons, muuungano wa madaktari wa kike wa upasuaji, ambapo kwa pamoja wanawanasihi wasichana wanaotamani kujiunga na taaluma hii barani. Tayari wana wanafunzi 150 wa kike kutoka sehemu tofauti barani Afrika.
Kwa sasa Dkt Mutebi anazidi kupata mafunzo ya urubani.
“Ndoto yangu mwanzoni ilikuwa kuwa daktari anayetoa huduma kwa kusafiri katika sehemu za mbali kwa kutumia ndege, yaani ‘flying doctor’, lakini kozi hiyo ilikuwa ghali sana,” aeleza.
Anatumai kutimiza hiyo ndoto kwa kuunganisha urubani na taaluma yake ya udaktari, na hivyo kufikisha huduma za kimatibabu katika maeneo ya mbali.