Italia yanyorosha Ugiriki na kujikatia tiketi ya Euro 2022
Na MASHIRIKA
ROMA, ITALIA
ITALIA walijikatia tiketi ya kushiriki fainali za Euro 2020 baada ya kuwazamisha Ugiriki kwa mabao 2-0 jijini Roma mnamo Jumamosi.
Baada ya kuumiza nyasi bure katika kipindi cha kwanza, kiungo Jorginho wa Chelsea aliwafungulia Italia ukurasa wa mabao kupitia kwa mkwaju wa penalti dakika ya 63.
Penalti hiyo ilitokana na tukio la Andreas Bouchalaki kunawa mpira ndani ya kisanduku cha lango la Ugiriki.
Federico Bernardeschi alitokea benchi katika dakika ya 68 na kuwafungia Italia bao la pili katika dakika ya 78.
Ni ushindi uliowakweza Italia hadi kileleni mwa Kundi J kwa alama 21 huku pengo la pointi 11 likitamalaki kwa sasa kati yao na Armenia wanaofunga orodha ya tatu-bora kundini.
Ugiriki walikuwa katika ulazima wa kusajili ushindi dhidi ya Italia ili kuweka hai matumaini ya kuwapiku Bosnia, Armenia na Finland- na hatimaye kufuzu.
Kwingineko, Jamhuri ya Ireland waliendeleza rekodi yao ya kutoshindwa katika kampeni za kufuzu kwa fainali za Euro 2020 baada ya kuambulia sare tasa dhidi ya Georgia.
Chini ya kocha Mick McCarthy, Ireland walikosa kabisa kulenga shabaha ya wapinzani wao katika kipindi cha kwanza huku wakionekana kuzidiwa maarifa katika takriban kila idara.
Matokeo hayo yanawasaza Ireland kileleni mwa Kundi D kwa alama 12 sawa na Denmark ambao pia wametandaza jumla ya mechi sita.
Ushindi kwa Ireland katika mchuano wa kesho utakaowakutanisha na Uswisi jijini Geneva utawahakikishia tiketi ya kushiriki fainali za Euro mwakani.
Wakijivunia mabao sita pekee kutokana na mechi sita, Ireland kwa sasa wana rekodi mbovu zaidi ya ufungaji tangu wabanduliwe kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizoandaliwa nchini Urusi mwaka 2018.
Ireland walishuka dimbani wakipigiwa upatu wa kuwachabanga Georgia kirahisi hasa ikizingatiwa rekodi yao ya awali.
Hadi walipovaana wikendi iliyopita, Ireland walikuwa wamewapepeta Georgia mara tisa na kuambulia sare mbili katika jumla ya mechi 11 zilizopita.
Ireland kwa sasa hawajapoteza mchuano wowote kati ya tisa iliyopita katika mapambano yote ya awali.
Mabao manane
Hata hivyo, wamefunga mabao manane pekee kutokana na mechi 13 zilizopita.
Wakati uo huo, Sergio Ramos aliingia katika mabuku ya historia kwa kuwa mwanasoka wa kiume kutoka bara Ulaya aliyewajibishwa kwa mara nyingi zaidi na timu yake ya taifa baada ya kuongoza Uhispania kusajili sare ya 1-1 dhidi ya Norway mnamo Jumamosi.
Mechi 168 ambazo Ramos amepigia Uhispania kwa sasa zinamfanya kumpiku kipa Iker Casillas na kuikaribia rekodi ya kiungo Ahmed Hassan aliyewachezea Misri michuano 184 kati ya 1995 na 2012.
Saul Niguez aliwafungia Uhispania bao la kwanza kabla ya jitihada zake kufutiliwa mbali na Josh King kupitia mkwaju wa penalti mwishoni mwa kipindi cha pili.
Uhispania kwa sasa wanaselelea kileleni mwa Kundi F kwa alama 19, tano zaidi kuliko Uswidi ambao ni wa pili. Ushindi kwa Uhispania katika mchuano wa Jumanne dhidi ya Uswidi utawawezesha kufuzu kwa fainali za Euro 2020.