Habari

Mwanaharakati afika kortini kupinga ripoti ya jopo la BBI

October 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na ABIUD OCHIENG

JOPO la maridhiano lililoundwa na Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga (BBI) limepinga mpango unaotishia kulizuia kuwasilisha ripoti yake kwa Rais kabla ya mwezi Oktoba kukamilika.

Bw Paul Mwangi ambaye ni mmoja wa makatibu wa jopo hilo pamoja na mwenzake, Bw Martin Kimani, wamesema walifanya kila juhudi kushirikisha umma katika shughuli za jopo hilo kitaifa hadi sasa ambapo wamekaribia kukamilisha ripoti yao inayojumuisha maoni ya wananchi na wadau mbalimbali.

Walisema hayo kortini baada ya mwanaharakati Moraa Gesicho kuwasilisha kesi kutaka jopo hilo lizuiwe kuwasilisha ripoti yake hadi itakapoamuliwa iwapo shughuli zake zilifuata sheria.

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Oktoba 16.

“Ripoti yetu imekamilika na sasa inafanyiwa uhariri kisha iwasilishwe kwa Rais. Wakenya wanasubiri kwa hamu kuisoma baada ya kutoa maoni yao kuhusu yale wanayotaka yafanywe kuboresha nchi ya Kenya,” akasema Bw Mwangi.

Kulingana naye, fedha nyingi, muda na rasilimali zilitumiwa kufanikisha kazi za jopo hilo kitaifa ikizingatiwa kuwa walitembelea kaunti zote 47, na wakashauriana pia na mashirika 82 ya kitaifa.

Zaidi ya hayo, alisema kwamba walipokea maoni 1,733 kupitia kwa barua zilizotoka kwa Wakenya.

Mwanasheria Mkuu kupitia kwa wakili wa serikali Lydiah Ndirangu, pia alisema inastahili BBI iruhusiwe kukamilisha majukumu yake kwani agizo likitolewa kusimamisha kazi hizo, itakuwa sawa na kuenda kinyume na matarajio ya wananchi.

Bi Ndirangu alisema mlalamishi hajaonyesha wazi wala kutoa ushahidi wa kuthibitisha madai yake kwamba katiba ilikiukwa katika utekelezaji wa shughuli za jopo hilo.