• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
TAHARIRI: Kaunti zishughulike kuyakabili mafuriko

TAHARIRI: Kaunti zishughulike kuyakabili mafuriko

Na MHARIRI

MVUA inayoendelea kunyesha katika maeneo mengi ya nchi tayari imeanza kusababisha maafa.

Japokuwa haijaua binadamu, imeshabeba mifugo huku ikikatiza uchukuzi katika maeneo mengi ya mashambani.

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa imekuwa ikitoa ilani ya kutokea kwa mvua siku kadhaa mapema. Ilani hiyo huwa ya kutahadharisha umma na pia kuwapa wakuu wa idara mbalimbali kujiandaa kukabiliana na athari za mafuriko.

Ni wiki jana tu ambapo kulizuka maporomoko maeneo ya Murang’a. Wiki iliyoanza jana inaelekea kuwa ya dhiki kwa wakazi wengi wa Pwani, kutokana na kufurika kwa mito na kuzuia watu kusafiri kutoka eneo moja hadi lingine.

Utabiri wa Idara ya Hali ya Hewa unaonyesha mvua inatarajiwa kuendelea kunyesha katika maeneo mengi ya nchi.

Katika miji mingi, mvua inaponyesha kwa wingi husababisha hata vifo kutokana na watu kusombwa na maji au kuta za baadhi ya mijengo kuporomoka.

Katika jiji la Nairobi, kwa mfano, mashimo mengi ya kupitishia majitaka yamezibwa na uchafu. Wafanyikazi wa Kaunti wanaosafisha jiji hawajashughulika na kuzibua mashimo hayo.

Hali hiyo inashuhudiwa katika miji mingi mikubwa, huku mashimo hayo pia yakiwa chanzo cha maafa kwa watu katika maeneo ambako mifuniko yake iliibwa au kwa sababu nyingine, hakuna aliyejali kuyafunika tena.

Mbali na watu kutumbukia kwenye mashimo hayo, wanaweza kuvunjika miguu au hata kupoteza maisha.

Jambo hili la kukabiliana na athari za mvua tumekuwa tukilikariri kila msimu unapofika na huenda ikaonekana kama tunawakera wahusika.

Ukweli ni kwamba, usalama wa wananchi ndilojukumu kuu la kila aliyepewa mamlaka ya kuongoza umma.

Huu ndio wakati muafaka kwa maafisa wa kukabiliana na majanga kuwaondoa watu walio kwenye maeneo ambayo kawaida hukumbwa na maporomoko ya ardhi kunaponyesha. Wale wanaoishi kwenye kingo za mito na maeneo ya chini ambako maji huenda kwa kasi, yafaa wahamishwe sasa.

Kama ambavyo kinga inashinda tiba, wadau mbalimbali wanapaswa kuanza kutoa tahadhari na kuchukua hatua kuwaepusha watu na athari za mvua. Haitakuwa busara kusubiri watu waporomokewe na udongo ndipo tujitokeze kuwapatia mablanketi, neti za kuzuia mbu na usaidizi mwingine wa kibinadamu.

Kaunti zishughulike sasa kukabiliana na athari za mafuriko.

You can share this post!

Korti yamzuia DCI kufunga akaunti za kampuni ya pombe na...

WASONGA: Mutyambai akabiliane na maafisa majambazi

adminleo