Kimataifa

California yaamrisha vyuo vya umma kuruhusu uavyaji mimba

October 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na AFP

CALIFORNIA, Amerika

CALIFORNIA ndilo eneo la kwanza kuamrisha vyuo vikuu vyote vya umma kutoa matibabu ya uavyaji mimba, hatua inayofungua pazia la kupanuliwa kwa huduma hizo ambazo zinadhibitiwa kote nchini humo.

Matibabu hayo ni sharti yatolewe katika vyuo vikuu vyote 34 vya umma kufikia Januari 2023 baada ya Gavana Newson kutia sahihi “Mswada wa Haki ya Kupata Huduma kwa Mwanafunzi wa Chuo” mnamo Ijumaa.

Mifumo miwili ya vyuo vikuu vya umma— Chuo Kikuu cha California na Chuo Kikuu cha California State — kwa sasa hazitoa huduma za uavyaji mimba chuoni.

“Huku maeneo mengine na serikali zikirejea nyuma, kuzuia haki ya uzazi, humu California tunasonga mbele, tukipanua uwezo wa kupata huduma na kuimarisha haki ya mwanamke ya kuchagua,”

“Tunaondoa vikwazo kwa afya ya uzazi – kuongeza nafasi ya kupata huduma katika mabewa ya vyuo na kutumia teknolojia kuleta usasa katika jinsi wagonjwa wanavyotangamana na watoaji huduma,” alisema Newsom, mwanachama wa Democrat.

Sheria hiyo mpya itahitaji utathmini wa vituo vya afya vyuoni kubaini uwezo wao wa kutoa matibabu ya uavyaji mimba, ambayo ni mchakato unaofanywa katika awamu ya kwanza ya ujauzito unaohusisha tembe mbili zinazosababisha mimba kuavya.

Baada ya hapo shule zitaweza pia kununua vifaa kama vile mashine za ultrasounds, na kuwafunza wahudumu jinsi ya kutumia mitambo hiyo na kanuni husika.

Hatua hiyo imejiri huku kukiwa na sheria kali za kuzuia ambazo zimetekelezwa katika maeneo kadha yanayopinga shughuli hiyo kote nchini.

Sheria hizo zimechukua aina mbalimbali ikiwemo kadha zinazofahamika kama miswada ya “mpigo wa moyo” ambazo zingezuia uavyaji mimba wakati mpigo wa moyo unapogunduliwa.