Orengo ataka Raila asitishe muafaka na Uhuru
Na JUSTUS WANGA
CHAMA cha ODM sasa kinamtaka kiongozi wake Raila Odinga kusitisha ushirikiano wake na Rais Uhuru Kenyatta kutokana na masaibu yanayomkumba mwanaharakati Miguna Miguna.
Wakiongozwa na wakili James Orengo na Katibu Mkuu wa chama hicho, Edwin Sifuna, viongozi hao wa chama walisema Rais amekataa kutekeleza mageuzi waliyoafikiana katika muafaka huo kwa kuendeleza maovu kadha kama ukiukaji wa amri za mahakama na kuhangaishwa kwa Miguna.
“Kwa vile serikali ya Uhuru imekataa kuzingatia utawala wa sheria, hamna haja kwa Bw Odinga kuendelea kushirikiana naye,” Bw Orengo aliambia “Taifa Jumapili.”
Kuhangaishwa, na hatimaye kufukuzwa kwa Miguna, alisema, kunaashiria kuwa muafaka huu haukuwa na maana yoyote.
“Uhuru ndiye anawajibika kwa yale yanayoshuhudiwa nchini. Ushirikiano wowote naye hautakuwa na maana yoyote ikiwa maafisa wake wataendelea kupuuza maagizo ya mahakama.
Maafisa hao wanaabisha idara ya mahakama chini ya maagizo yake. Alionya idara ya mahakama ilipobatilisha ushindi wake na matokeo ya onyo hilo sasa yanaonekana na Wakenya wote,” Orengo ambaye ni Seneta wa Siaya alisema.
Akiunga mkono kauli ya Orengo, Bw Sifuna aliwataka Wakenya wa matabaka yote kujitokeza kutetea uhuru wa Idara ya Mahakama, utawala wa sheria na uzingatiaji wa maagizo ya mahakama.
“Kwa hivyo, ODM inatoa wito kwa Wakenya wenye nia njema, mawakili, mashirika ya kijamii na makanisa kujitokeza wiki ijayo na kuwakamata maafisa wakuu wa serikali waliokaidi amri ya mahakama,” akasema.
Bw Sifuna alikuwa akirejelea Waziri wa Usalama Fred Matiang’i, Inspekta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet na Katibu wa Wizara anayesimamia Idara ya Uhamiaji Gordon Kihalangwa ambao walikataa kufika mahakamani kufafanua sababu za wao kutomruhusu Wakili Miguna kuingia nchini.
Bw Odinga amekashifiwa na wafuasi wake ambao wanahisi alikosea kwa kubuni ushirikiano na Rais Kenyatta.
Wafuasi hao waliotuma jumbe kupitia mitandao ya kijamii wanahisi kuwa Bw Odinga anafaa kuendelea kuikosoa serikali kama zamani wakisema, Rais Kenyatta hajajitolea kutekeleza yale waliyokubaliana Machi 9.
Kauli ya Orengo na Sifuna inajiri wakati ambapo Bw Odinga ametengwa na vinara wenzake katika NASA; Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula waliokerwa kwa kuachwa nje katika muafaka huo.
UKINZANI
Hata hivyo, baadhi ya wandani wa Bw Odinga wanatofautiana na kauli ya Orengo na Sifuna wakimtaka kuendelea kushirikiana na Rais Kenyatta.
“Nadhanii Bw Orengo anapaswa kulaumu mahakama kwa kushindwa kuhakikisha kuwa maagizo yake yanatekelezwa. Suala hilo halina uhusiano wowote na muafaka kati ya Rais na Bw Odinga,” akasema Mbunge mmoja ambaye ni mwandani wa Odinga.
“Malalamishi hayo hayana msingi wowote… wanafaa kufahamu kuwa masaibu ambayo Miguna anapitia ni ya kujitakia.
Hayana uhusiano wowote na muafaka kati ya viongozi hao wawili ambao ulilenga kutuliza joto la kisiasa nchini kwa ajili ya maendeleo,” akasema Mbunge huyo kutoka Nyanza Kusini anayehudumu kipindi cha pili.
Naye Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, John Mbadi vile vile ameanza kushuku ukweli uliopo katika ushirikiano kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga akisema huenda utulivu ulioshuhudiwa nchini tangu wawili hao waliposalimiana ukayeyuka.
“Kudhalilishwa kwa Miguna katika uwanja wa ndege wa JKIA na kufurushwa kwake kwa mara ya pili kunaibua wasiwasi kuhusu uhalali wa muafaka huu,” akasema mbunge huyo wa Suba Kusini.
Naye Mbunge Maalumu wa ANC Godfrey Osotsi alisema taarifa ya pamoja iliyotiwa saini na Rais Kenyatta na Bw Odinga na kusomwa nje ya jumba la Harambee, ilisisitiza uzingatiaji wa utawala wa sheria ambayo sasa serikali inakiuka.
“Kupitia salamu hizo, kiongozi wetu Raila Odinga alijitolea kupalilia amani na uthabiti nchini lakini sasa ni wazi kuwa serikali ya Kenyatta ilikuwa ikituhadaa,” akasema mbunge huyo.