• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
Wanaume wanafariki kwa wingi katika ajali za barabarani kuliko wanawake, NTSA yafichua

Wanaume wanafariki kwa wingi katika ajali za barabarani kuliko wanawake, NTSA yafichua

Na MARY WAMBUI na CHARLES WASONGA

IDADI ya wanaume wanaofariki katika ajali za barabarani ni juu ikilinganishwa na ile ya wanawake, ripoti ya Mamlaka ya Kitaifa kuhusu Usalama Barabarani (NTSA) imefichua.

Kulingana na ripoti hiyo iliyotolewa Jumanne, jumla ya wanaume 2263 walipoteza maisha yao katika ajali za barabarani kati ya Januari na Oktoba 7, 2019, ikilinganishwa na 1927 waliofariki wakati kama huo mwaka 2018.

Na Kenya ilipoteza wanawake 427 katika mwaka wa 2019 ikilinganishwa na 405 katika mwaka wa 2018 katika kipindi kama hicho.

NTSA ilisema kuwa nyingi za ajali hizi hutokea siku za wikiendi, Jumapili ikiongoza ikifuatwa na Jumamosi kisha siku za Ijumaa.

Kulingana na ripoti hiyo, ajali nyingi hutokea kati ya saa kumi na moja jioni na saa mbili za usiku na husababishwa na makosa ya madereva na watumiaji wengine wa barabara.

Vifo hivyo hutokana na visa vya watu kugongwa na magari kisha yakatoweka, madereva kupoteza udhibiti wa magari yao, magari kupitana bila kutahadhari, uendeshwaji wa magari kwa kasi, miongoni mwa njia nyinginezo.

Kulingana na umri, wanawake na wanaume wenye umri wa kati ya miaka 30-34 walisababisha idadi kubwa ya ajali wakifuatwa na watu wenye umri wa kati ya miaka 25-29 na miaka 39.

Vilevile, ilibainika kuwa wanaume wenye umri wa miaka ya 65 kwenda juu ndio madereva waangalifu sana barabarani kwa sababu idadi ya ajali zilizosababisha wa watu wa umri hiyo ilikuwa ndogo zaidi.

Kaunti ambazo zinaongoza katika visa vya ajali ni Nairobi iliyoandikisha ajali 344, Kiambu (233) na Nakuru ambayo iliandikisha ajali 187 katika kipindi hicho.

You can share this post!

Wapwani walalama kuchezewa na serikali

Wakenya waibuka kuwa wakarimu zaidi Afrika

adminleo