WASIA: Jinyime kisha ujitume ili kufikia upeo wa maazimio yako maishani
Na HENRY MOKUA
WANAFUNZI wengi wa enzi hizi wana ndoto za kupigiwa mfano sawa na watangulizi wao.
Wanayo tamaa ya kuvunja rekodi za watangulizi wao na kuweka rekodi mpya zitakazowatambulisha kwenye ramani za vijiji vyao, magatuzi yao, maeneo yao na hata nchi zao.
Wanafunzi hawa, kama wanafunzi wengine wowote hupenda kupongezwa, hata kutuzwa kwa kila jitihada ndogo wanayodhihirisha.
Isitoshe, hutegemea daima kwamba yupo mtu, japo hawamjui wala kukisia ni nani, atakayewaelekeza kugundua na kuviendeleza vipaji vyao. Mbona wengi wao hawafanikiwi lakini?
Asilimia kubwa ya wanafunzi hupenda kufanya mambo kikawaida tu, hupendelea kusalia katika kiwango cha wastani na huchukia kujinyima starehe ili kufanikiwa.
Kila mwalimu, mzazi au mwangalizi mwingine anapowataka kujihini, wanafunzi hawa hujibu kwa ukaidi na ujeuri wao. Kwa kuyajua machache yanayozidi umri wao, hufikiri kwamba sasa wapo katika ngazi moja na wakubwa zao.
Harakati hizi huwasababisha baadhi ya walimu na wazazi kuwapa wanafunzi wanaohusika fursa ya kujaribu mkondo wao wa mawazo hadi utakapowafikisha.
Hugundua miaka kadhaa baadaye kwamba wamepoteza fursa za pekee ambazo hazitawarudia tena. Ushindi wa Eliud Kipchoge wikendi iliyopita una mengi kwetu kujifunza. Hebu tuangazie baadhi yayo:
Mosi, sharti ukiuke ukawaida ili kutambuliwa. Tia bidii katika kila ulitendalo uone ni kwa lipi matokeo yako yanadhihirisha upekee. Ukifanya kila jambo kikawaida tu, matokeo yatakuwa ya kawaida na huenda usigundue hata talanta ambayo ingeyabadilisha maisha yako.
Tenga muda zaidi kufanya jambo ambalo unalithamini, shauriana na wajuzi wa jambo hilo ili ujifunze namna ya kulifanya tofauti na hivyo kupata matokeo tofauti.
Kipchoge alipenda kukimbia hata akakufanya kukimbia kama uraibu wake. Ikiwa somo la Fizikia linakuwia jepesi, koma kuridhishwa na asilimia 50 kwalo.
Badala yake, lifanyie mazoezi na kushauriana na mwalimu wako wa somo hilo au hata mwanafunzi mwenzio anayefanya vyema kwalo, uandikishe matokeo yatakayodhihirisha ubingwa wako kwalo.
Iwapo unapenda kuimba, imba kana kwamba unaimba kwa mara ya mwisho kila upatapo fursa; ni kwa hivi unaweza kupata matokeo ya kupigiwa mfano na kuanza kuipiga msasa talanta yako mpya.
Pili, jiwekee malengo na shabaha. Malengo ni muhimu mno kwa kila atakaye kufanikiwa. Taja angalau jambo moja unalotaka kulifikilia au kuligundua katika kila zoezi unalolifanya.
Aidha jiwekee shabaha yenye kufikilika ili ikupe hamasa ya kuendelea mbele zaidi. Jiambie kwamba ‘kila mwanadamu ana uwezo usiokadirika’ kaulimbiu ambayo ilimpa bingwa Kipchoge uwezo wa kujiamini hadi akavunja rekodi yake mwenyewe na kuingia katika vitabu vya Historia upya.
Uwezo
Tumia uwezo wako kama kigezo badala ya kushindana na wenzio. Kumbuka, Eliud alikuwa na hiari ya kusalia na rekodi yake ya awali ya kukimbia masafa ya kilomita 42 kwa saa 2 na sekunde 25 kwani hamna mwingine ulimwenguni aliyewahi kukimbia kwa kasi hiyo katika mbio zenyewe.
Hata hivyo, uwezo wake ulimpa kujaribu kuivunja rekodi yake mwenyewe; kujiamini kwake kukawa msingi wa matokeo yake ya kustaajabisha Jumamosi iliyopita ambapo alitumia muda wa saa 1, dakika 59 na sekunde 40 kukamilisha mbio hiyo.
Hii ilikuwa sawasawa na shabaha yake ya kutumia chini ya muda wa saa 2 kuikamilisha.
Mwisho na muhimu zaidi, usimtarajie yeyote kukushika mkono, kukujenga katika siku za awali. Jitume ukijua kwamba Mwenyezi Mungu mwenyewe aliyekupa uwezo ndiye atakayekufanikisha.
Hii imani ya vijana wengi siku hizi kutambuliwa kutoka kwenye umati wakati wakifanya mambo kikawaida na kusalia katika kiwango cha wastani ni imani potovu. Jitenge na umati, jijenge kiasi cha kutambuliwa, zidi kujijenga na utakuwa nyota wa kaunti yako, eneo lako, nchi yako au hata ulimwengu mzima – hapo ndipo juhudi zako za awali zilizokosa kutambuliwa zitajulikana na kulipwa. Usisahau unyenyekevu lakini! Licha ya kuwa bingwa wa ulimwengu mzima, Kipchoge hajakoma kumthamini, kumsikiliza kocha wake.