Makala

Wanawake walilia usawa katika Bodi za Mashamba

October 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na LAWRENCE ONGARO na LEONARD ONYANGO

WANAWAKE zaidi ya 100 kutoka kaunti tofauti nchini, Jumanne walikongamana jijini Nairobi ili kujadili maswala mengi yanayowahusu katika maisha yao ya kila siku.

Mkutano huo wa Siku ya Kimataifa ya Wanawake Mashinani ulijadili, pamoja na mambo mengine, masaibu mengi wanayopitia.

Wanawake hao walikuwa wakitathmini mambo ambayo wameweza kunufaika nayo tangu kongamano la wanawake lililofanyika Beijing, China miaka 25 iliyopita.

Wanawake hao walisema siku hiyo ilikuwa muhimu kwao kwa sababu imebainika pakubwa ya kwamba kote ulimwenguni mwanamke ameshikilia sehemu kubwa katika maendeleo yanayoshuhudiwa mahali pengi.

Walitoa mfano wa kilimo ambayo ikitazamwa kwa undani utapata ya kwamba wanawake wengi wanazamia katika mashamba yao katika vijijini lakini kazi kubwa wanayofanya haitambuliki kirasmi.

Bi Jael Amati ambaye ni mpatanishi wa vikundi vya wanawake kwenye Shirika la Grassroots Organisations Operating Together in Sisterhood (Groots)-Kenya alisema mwanamke kote ulimwenguni amewekewa mzigo mzito mabegani mwake kwani unapozuru vijijini, utapata ya kwamba mwanamke ndiye analea watoto, anamtayarisha mumewe, anakwenda shambani, anatafuta maji mtoni, analinda wazee, anatunza boma, na majukumu mengine mengi ambayo hayawezi kutajwa yakamalizwa.

“Sisi wanawake tunafanya makubwa ambapo hata kama ni kupima thamani ya kazi hiyo bila shaka haiwezekani. Kwa hivyo, tungetaka majukumu hayo yaweze kutambulika na yasichukuliwe kwa wepesi hivyo,” alisema Bi Amati.

Alisema asilimia kubwa ya kazi za sulubu zinazotekelezwa na wanawake zinastahili  kutambulika na serikali.

Alisema imefika wakati ambapo wanawake wanastahili kutambulika katika nyadhifa kubwa serikalini kwa sababu wengi wao wana uwezo wa kufanya majukumu kadha yanayotekelezwa na wanaume.

Bi WinRose Mwangi kutoka Kaunti ya Laikipia ambaye anatetea maslahi ya wanawake mashinani kupitia Shirika la Groots Kenya, alisema wanawake wanastahili kupigania haki zao ili pia waingie uongozini.

“Sisi kama wanaweke ni vyema tuwe katika mstari wa mbele ili pia maslahi yetu yaeleweke na kupewa kipaumbele,” alisema Bi Mwangi.

Uchunguzi uliofanywa na Shirika la Groots Kenya umebainisha ya kwamba Mwanamke bado hajapata haki yake ipasavyo katika uongozi wa nchi hii.

Walitaja afisi za bodi ya mashamba waliyosema haina uwakilishi ufaao wa maafisa wanawake. Wakati huo pia sio wanawake wengi wanapata vyeti miliki vya mashamba yao hata wakati waume wao wanapoaga dunia.

Wanawake hao kwa kauli moja walikubaliana ya kwamba ni vyema wapewe hamasisho ili wawe na njia mwafaka wa kupata mikopo ya hazina ya Uwezo Fund, Women Enterprise Fund (WEF), na hata GAAF Funds.

Walipendekeza pia wapewe hamasisho jinsi ya kutumia vifaa vya kisasa katika mashamba yao ili waweze kupata mazao za kulisha familia bila shida ya ukame.

Ilidaiwa ya kwamba kati ya mwaka wa 2013-2017, serikali ilitoa hati miliki za ardhi 3 milioni na mingoini mwa idadi hiyo asilimia 10.3 ilipewa wanawake huku wanaume wakifikisha asilimia 85.

Wanawake wamemtaka Waziri wa Ardhi Farida Karoney kuhakikisha kuwa kuna usawa wa kijinsia katika bodi za kusimamia mashamba katika kaunti ili waweze kuwazuia wanaume kuuza ardhi kiholela.

Wakizungumza jijini Nairobi ambapo mamia ya wanawake kutoka kaunti mbalimbali walikongamana kuadhimisha Siku ya Kimataifa kuhusu Wanawake wanaoishi Vijijini, wanawake hao walishutumu manaibu makamishna wa kaunti kwa kuteua wajumbe wa bodi hizo kisiri.

“Muda wa kuhudumu kwa wajumbe wa bodi wa sasa umekamilika na shughuli ya kuteua wajumbe wapya imeanza. Lakini uchunguzi wetu umebaini kwamba manaibu kamishna wa kaunti wanafanya uteuzi kisiri badala ya kutangaza nafasi hizo,” akasema Bi Esther Amati, Mshirikishi wa Miradi wa shirika la kupigania ustawi wa wanawake wa vijijini linalojulikana kama Grassroots Organisations Operating Together in Sisterhood (Groots)-Kenya.

Bodi za Kusimamia Ardhi zilibuniwa na Sheria ya Usimamizi wa Mashamba ya 1967 na zimetwika jukumu la kuidhinisha au kutupilia mbali uuzaji, ubadilishanaji au ugavi wa ardhi inayotumika katika kilimo.

Kwa kuwa bodi hizo hujumuisha wenyeji, huwa rahisi kugundua walaghai wanaojaribu kuuza mashamba ya watu wengine bila idhini.

Japo Waziri wa Ardhi ndiye amepewa jukumu la kuteua wajumbe wa bodi hizo, manaibu kamishna wa kaunti ndio wana usemi kuhusu mtu anayefaa kuwa mjumbe wa bodi.

“Waziri anafaa kuweka mwongozo ambao utahakikisha kuwa shughuli ya uteuzi wa wajumbe wa bodi hizo ina uwazi. Wanawake wa vijijini wanahitaji kuwa kwenye bodi hizo ili kuzuia viasa ambapo wanaume wamekuwa wakiuza mashamba ya kifamilia bila idhini ya wanawake,” akasema.

Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na shirika la Kenya Land Alliance wiki iliyopita ilibaini kuwa bado kuna pengo kubwa la umiliki wa ardhi baina ya wanawake na wanaume.

Ripoti hiyo ilionyesha kuwa chini ya asilimia tano ya wanawake kutoka Kaunti za Kisumu na Siaya wanamiliki mashamba.

Ripoti hiyo pia ilibaini kuwa kati ya hatilimiliki milioni 3 zilizotolewa na Rais Uhuru Kenyatta kati ya 2013 na 2017, wanawake walipata asilimia 10.