Habari

Jumwa kujua hatima yake leo Alhamisi kuhusu mauaji Kilifi

October 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BRIAN OCHARO

MBUNGE wa Malindi Aisha Jumwa, alipanga kuvuruga uchaguzi mdogo wa Wadi ya Ganda, Kaunti ya Kilifi ambako mtu mmoja aliuawa Jumanne, mahakama ya Mombasa ilifahamishwa Jumatano.

Mbunge huyo na mlinzi wake Geofrey Okuto, walikesha katika seli za polisi kwa siku ya pili baada ya kukamatwa kufuatia ghasia hizo nyumbani kwa mgombeaji wa chama cha ODM kwenye uchaguzi huo mdogo, mnamo Jumanne jioni.

Mahakama iliagiza wazuiliwe hadi leo Alhamisi itakapoamua iwapo itaruhusu polisi wawazuilie kwa siku 21 wakamilishe uchunguzi.

Maafisa wa polisi waliambia mahakama kwamba wawili hao wanachunguzwa kwa mauaji ya Gumbao Jola, mjomba wa mgombeaji wa chama cha ODM kwenye uchaguzi huo mdogo wa Ganda, Bw Reuben Mwambize Katana. Kiongozi wa mashtaka Alloys Okemo, alisema wapelelezi wanamchunguza mbunge huyo kwa mauaji, kuchochea ghasia na kushambulia wananchi.

“Wapelelezi wanachunguza kubaini ikiwa mshtakiwa alitenda kosa linalohusiana na uchaguzi na ukiukaji wa sheria za uchaguzi alipovamia mkutano akiwa na walinzi na wafuasi wake,” Bw Okemo aliambia mahakama.

Alimtaja Bi Jumwa kama mchochezi na mpenda ghasia, akisema alivamia boma la Bw Katana akiwa katika msafara wa magari akiandama na walinzi wake na kuwavuruga zaidi ya watu 500 waliokuwa mkutanoni. Ripoti zinasema kuwa walipomuona mbunge huyo na walinzi wake, walianza kuwakemea na kuwarushia mawe na vifaa butu.

“Mlinzi wake alifyatua risasi kadhaa na katika hali hiyo, umati ulianza kupiga kelele ukidai kuwa Bw Jola alikuwa ameuawa, umati ulianza kuzua ghasia na kufanya maafisa wa polisi waliokuwepo kuutawanya kwa kufyatua risasi hewani,” Bw Okemo alieleza mahakama.

Kuvuruga uchaguzi

Hati ya kiapo iliyowasilishwa na Inspekta Mkuu wa Polisi Joseph Wambua inaeleza kuwa ripoti za kijasusi zilisema mbunge huyo na wafuasi wake walipanga kuvuruga uchaguzi mdogo wa Ganda unaofanyika leo Alhamisi.

“Maafisa wa usalama eneo hilo wana habari za kuaminika kuwa wafuasi wa Jumwa huko Takaungu wanapanga kuvuruga uchaguzi mdogo. Yeye ni mbunge wa Malindi na kwa hivyo ana ushawishi na anaweza kuingilia uchunguzi kwa kuwashawishi mashahidi,” kiongozi wa mashtaka alieleza.

Alisema mbunge huyo na mlinzi wake wanafaa kuzuiliwa kwa sababu usalama wao uko hatarini ikizingatiwa kuwa umati uliokusanyika katika kituo cha polisi cha Malindi alikozuiliwa kwa muda ulikuwa ukitaka damu yake.