Mahujaji 35 wafa katika ajali Medina
Na MASHIRIKA
RIYADH, SAUDI ARABIA
RAIA 35 wa kigeni waliuawa na wengine wanne wakajeruhiwa wakati basi moja liligongana na trela katika jiji takatifu la Medina, vyombo vya habari nchini Saudi Arabia viliripoti Alhamisi.
Basi hilo, ambalo lilikuwa linawasafirisha mahujaji liligongana na trela hilo ana kwa ana katika jiji hilo lililoko Magharibi mwa taifa hilo la Kifalme kabla ya kulipuka na kuteketea, msemaji wa polisi wa Medina alisema kulingana na shirika la habari la Saudi Press Agency (SPA).
Waliohusika katika ajali hiyo walikuwa mahujaji kutoka mataifa ya Kiarabu na yale ya bara Asia, shirika hilo lilisema.
Vyombo vya habari vilibeba picha za basi hilo likiteketea huku madirisha yake yakiwa yemeng’olewa.
Waliojeruhiwa walikimbizwa katika Hospitali ya Al-Hamna huku uchunguzi ukianzishwa kubaini chanzo cha ajali hilo. Gazeti la Okaz lilisema wahasiriwa walikwua wageni ambao wanaishi nchini humo na ambao waalikuwa wanafanya shughuli ya kidini inayojulikana kama umrah -kutembelea maeneo matakatifu kulingana na dini ya Kiislamu, shughuli ambayo inaweze kuendeshwa mwaka mzima.
Mwaka huu jumla ya waumini milioni 2.5 wa dini ya Kiislamu kutoka kote ulimwenguni walikongamana nchini Saudi Arabia mnamo Agosti kushiriki shughuli ya kila mwaka ya Hajji- mojawapo ya nguzo tano za dini hiyo.
Shughuli za Hajj na Umrah hufanyika mjini Mecca na maeneo ya karibu ya milima na mabonde, magharibi mwa nchi hiyo. Hata hivyo, baadhi ya mahujaji pia huendesha shughuli katika jiji takatifu la Medina.
Mwaka jana, reli ya treni ya kasi inayounganisha Mecca na Medina ilizinduliwa kurahisisha usafiri kati ya miji hiyo miwili, kwa muda mfupi wa saa mbili na nusu. Zamani safari kati ya miji hiyo miwili ilichukua muda wa saa tano.
Salamu za pole
Mwanamfalme Faisal bin Salman, gavana wa eneo la Medina, alituma salamu za pole kwa jamaa na familia za wahanga wa ajali hiyo, SPA ilisema.
Japo uraia wa baadhi ya waliofariki haikujulikana, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi pia alituma pole zake.
“Nimepokea habari za ajali ya basi karibu na Mecca nchini Saudi Arabia kwa huzuni kubwa. Natuma rambirambi zangu kwa familia zilizopoteza wapendwa wao. Nawaombea waliojeruhiwa ili wapate afueni ya haraka,” akasema kupitia ujumbe kwenye ukurasa wa akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter.
Usafirishaji wa waumini katika maeneo matakatifu, hasa wakati wa hajji, hukumbwa na changamoto kubwa nchini Saudi Arabia.
Msongamano mkubwa wa magari hushuhudiwa barabarani kutokana na ongezeko la mabasi ya kuwasafirisha wageni.
Mamilioni wa waumini wa dini ya Kiislamu wamekuwa wakitembelea Saudi Arabia kuhiji kila mwaka, hatua ambayo taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta huchukulia kama njia kutumia sherehe hiyo ya kidini kama njia ya kipiga jeki sekta yake ya utalii.